Katika kile kinachotafsiriwa kuwa ni kusafisha idara zilizopo ndani ya
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko
katika Idara ya Uhamiaji baada ya kumteua
Johari Masoud Sururu kuwa Kamishna
mpya wa Zanzibar.
Uteuzi huo wa Rais Kikwete umekuja siku moja tangu alipomteua Kamishna wa
Polisi, Hamdan Omari Makame kushika wadhifa huo Zanzibar huku aliyekuwa
akishikilia nafasi hiyo, Kamishna Mussa Ali Mussa akiteuliwa kushika wadhifa
mpya wa Kamishna wa Polisi Jamii.
Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Isaac Nantanga ilieleza kuwa kutokana na uteuzi huo, aliyekuwa Kamishna wa
Uhamiaji Zanzibar, Mwinchumu Hassan Salim atapangiwa kazi nyingine. Kabla ya
uteuzi huo ambao umeanza Novemba 24 mwaka huu, Sururu alikuwa Mwambata wa
Uhamiaji katika Ubalozi wa Tanzania, Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu
(UAE).
Agosti 28 mwaka huu baada ya kuongozana kwa matukio ya watu kukamatwa na
dawa za kulevya na meno ya tembo katika viwanja vya ndege nchini, nje ya nchi
na maeneo mbalimbali, Rais Kikwete alifanya mabadiliko katika idara hiyo kwa
kumteua Sylvester Mwakinyule kuwa Kamishna Mkuu, Idara ya Uhamiaji.
Mwakinyule alichukua nafasi ya Magnus Ulungi ambaye ilielezwa kuwa
atapangiwa kazi nyingine. Kabla ya uteuzi huo, Mwakinyule alikuwa Naibu
Kamishna wa Uhamiaji na Mwambata wa Uhamiaji katika Ubalozi wa Tanzania,
London, Uingereza.
Katika uteuzi wa juzi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko katika idara
nyingine ya wizara hiyo kwa kuwapandisha vyeo maofisa waandamizi wanne wa Jeshi
la Polisi, pamoja na kufanya uteuzi wa nafasi za madaraka kutokana na
mabadiliko ya muundo wa jeshi hilo. Waliopandishwa vyeo ni pamoja na Isaya
Mungulu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI)
kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Robert Manumba ambaye amestaafu.
Awali, Mungulu alikuwa Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini (CID) na baada ya
Manumba kustaafu Novemba 11 mwaka huu, aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo.
Maofisa wengine waliopandishwa vyeo kuwa Makamishna wa Polisi (CP) ni Ernest
Mangu, Thobias Andengenye, Abdulrahaman Kaniki na Makame.
Rais Kikwete pia amempandisha cheo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) Athuman Diwani kuwa Naibu Kamishna wa Polisi na kumteua kuwa Naibu DCI.
Walioteuliwa katika nafasi za madaraka ni Clodwig Mtweve (Kamishna wa Fedha
na Utaratibu wa Ugavi na Usafirishaji wa Watu na Vitu (Logistics), Paul
Chagonja (Kamishna wa Operesheni na Mafunzo).
Mangu (Mkurugenzi wa Usalama wa Jinai), Andengenye (Kamishna wa Utawala na
Utumishi) na Kaniki (Uchunguzi wa Ushahidi wa Jinai).
safi sana jk
ReplyDelete