Monday, 9 December 2013

DK.TITUS KAMANI ADAIWA KUMDANGANYA JK

Filled under:



MBUNGE wa Busega mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani (CCM) anadaiwa kumdanganya Rais Jakaya Kikwete kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni mwake.

Inadaiwa kwamba hivi karibuni Rais Kikwete akiwa ziarani Busega, alikabidhiwa na mbunge huyo kitabu cha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenye kurasa 22 kinachoelezwa kwamba taarifa hiyo imechakachuliwa.

Baadhi ya wakazi wa Busega walizungumza na walidai baadhi ya miradi iliyoainishwa katika kitabu hicho hajaitekelezwa kipindi cha Dk. Kamani, kwamba ilitekelezwa kati ya mwaka 2005 na 2010.

Walidai kwamba ipo miradi kadhaa ilitekelezwa na aliyekuwa Mbunge wa zamani, Dk. Raphael Chegeni (CCM), lakini katika kitabu hicho imetajwa kwamba utekelezwaji wake ulifanyika kati ya mwaka 2011/2012.

Minza Edward na Hoka Manoni waliutaja mradi wa mwalo wa Ihale uliopo kwenye Kata ya Kaloleli ulikamilika na ulifunguliwa rasmi na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Awamu ya Tatu, Dk. Ali Mohamed Shein mwaka 2009.

Ilidaiwa kwamba mradi wa umeme vijijini wa Rea katika mji wa Lamadi, nao ulitekelezwa kati ya mwaka 2008/2009 na sio 2011/2012 kama ilivyoelezwa kwenye kitabu alichokabidhiwa Rais Kikwete.

Mradi mwingine ni ujenzi wa zahanati kwenye Kata ya Mwamanyili unaotajwa kugharimu sh milioni 3.1. Diwani wa kata hiyo, Charles Luyenze alisema: “Huu mradi umetekelezwa mwaka 2010, na aliyekuwa mbunge wakati huo aliujenga kwa sh milioni 3. Dk. Kamani alichangia sh 100,000.”

Dk. Kamani alipotafutwa  kwa simu yake ya kiganjani ili atoe ufafanuzi juu ya madai hayo, iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) hakujibu.

0 comments:

Post a Comment