Monday, 9 December 2013

MKUU WA KITUO CHA POLISI IGUNGA ADAIWA KUMTOROSHA MTUHUMIWA

Filled under:

SAKATA la Mkuu wa Kituo cha Polisi Igunga mkoani Tabora (OCS), SP Edson Mafuru, kudaiwa kumtorosha mtuhumiwa  Magaka Singu aliyempa mimba mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Hani Hani, limechukua sura mpya baada ya mama mzazi wa mtuhumiwa kudai fedha zilizotolewa na  mwanae kwa polisi zirudishwe kabla hawajamkamata.

Wakati mama huyo akidaiwa kutoa vitisho hivyo kwa polisi,  taarifa kuwa mtuhumiwa anaendelea na shughuli zake kama kawaida na jana alishiriki katika mnada wa hadhara uliofanyika Igunga mjini.

Hatua ya mtuhumiwa kushindwa kukamatwa kwa madai ya kukingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, inadaiwa kuleta hali ya mkanganyiko miongoni mwa askari na kufikia baadhi yao kutuhumu kuwa ujana walio nao ndiyo sababu ya kuwa na tamaa zinazokiuka maadili ya Jeshi la Polisi.

“Kuna taarifa kuwa OCS anachunguzwa na yeye anadai hahusiki, lakini ni askari wa kituo hiki hiki waliokwenda kumkamata mtuhumiwa na kumuweka ndani kabla hajatolewa, na kingine ni kwanini ayanunue magazeti yote yaliyoandika habari zake kama anona hana kosa?” alisema na kuhoji mtoa habari wetu katika Kituo cha Polisi Igunga.

Desemba 4 mwaka huu, gazeti hili liliandika habari ya SP Mfuru kudaiwa kumwachia mtuhumiwa Singu aliyefunguliwa jalada namba IG/1430/2013 na kisha mtuhumiwa huyo kukamatwa Novemba 10 kabla ya kuachiwa siku iliyofuata kwa dhamana ya shilingi laki 4.

Katika habari hiyo lilieleza masharti aliyopewa mtuhumiwa ili aachiwe kuwa ni kutoa kiasi cha shilingi milioni 3 ambazo alitoa kati ya Novemba 17 na 21, na kisha kutakiwa kuondoka katika mji wa Igunga kwa muda.

Kutokana na polisi wa Igunga kushindwa kumkamata mtuhumiwa,  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Peter Ouma na kumuuliza hatua walizochukua baada ya Mkuu wa Wilaya, Elibariki Kingu kuomba mkuu huyo wa kituo aondolewe katika wilaya yake kutokana na kukiuka agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuwadhibiti watu wanaowapa mimba wanafunzi.

Katika majibu yake, Ouma alisema kuwa suala hilo ni tuhuma na kwamba wanazifanyia uchunguzi.

Alipoulizwa juu ya namba ya jalada la kesi kama haina uhusiano na mtuhumiwa anayedaiwa kuachiwa na OCS Mafuru, Ouma alisema yupo safarini.

“Mimi nipo Moshi suala lenyewe ni tuhuma tu na sisi tunachunguza, tukikamilisha tutatoa taarifa,” alisema.

0 comments:

Post a Comment