Sunday, 7 September 2014

AL SHABAB WATANGAZA KIONGOZI MPYA BAADA YA KIFO CHA GODANE

Filled under:

Kundi la al-Shabab la nchini Somalia limemchagua Ahmed Umar (Ahmad Omar au Abu Ubaidah) kuwa mridhi wa Ahmed Abdi Godane (Abu Zubeyr) aliyeuawa katika mashambulizi yaliyoongozwa na Marekani siku ya Jumatatu kuamkia Jumanne ya wiki iliyopita.

Katika taarifa yake iliyonukuliwa na kituo cha habari cha Al Jazeera, kundi hilo limeapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya mmoja wa waasisi wao likisema kuwa kifo cha mwanazuoni na kiongozi wao kinawalazimu kujitwika mabegani jukumu la malipo ambalo hawataliangusha wala kulisahau bila kujali muda wa kulikamilisha.

Kundi hilo limethibitisha kuuawa kwa Godane na viongozi wake wengine wawili.

Godane aliongoza al-Shabab tangu mwaka 2008 baada ya kifo cha mtangulizi wake, Aden Hashi Ayro ambaye naye aliuawa baada ya mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani huko kusini mwa mji wa Dhusamareeb.

Mashambulizi ya Jumatatu yalifanywa kwenye ngome ya al-Shabab huko Barawe yakimlenga Godane ambaye mwaka 2012 aliwekewa dau la dola za Kimarekani milioni $7 kama malipo kwa yeyote ambaye angewezesha na kufanikisha kukamatwa au kuuawa kwake.

Rais wa Somalia amekaririwa akiwataka wanamgambo wa al-Shabab kujisalimisha huku akiwapa siku 45 za msamaha kwa wapiganaji watakaotii wito huo.

0 comments:

Post a Comment