Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni
heshima kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Ni katika nchi chache sana
duniani, mtoto wa maskini kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani akiuza
karanga, Big G, maandazi, jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata
chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi
yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari. Hii
inamaanisha misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa
Taifa hili haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na
inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe
kipaji chako.
Hili peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kuota
kuwa Rais – nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa
Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna
haki na fursa sawa bila kujali nani anatokea familia
ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni lazima atokee
kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania itakayodumu
kwenye misingi hii: kwamba sisi sote ni ndugu, na tuna fursa sawa.
Kwamba, kuendelea kimaisha na kibinafsi ni haki ya binadamu na si
hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie kama nilivyokuwa mimi hapa, ana
haki na fursa ya kuwa mbunge ama Rais wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa
Mbunge.
Kwa namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza
waasisi wa Taifa letu kwa kusimamia tunu hizi. Niwashukuru pia viongozi
wote walionitangulia kwa kuzilinda, na niahidi nitakuwa wa mwisho
kuisaliti nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo nimefika hapa kwa sababu chama change kina mfumo mzuri
ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na Wenyeviti waliomfuatia mpaka
na sisi tumeukuta. Leo nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na
wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara
iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya
kuwa Mbunge. Leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo
itatoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu yangu Kizaa Baba aliishi Kijijini Goweko, Mlimani, na alikuwa
mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe
waliishi maisha ya heshima sana pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala
kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani
ya Chama Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.
Babu yangu na Bibi yangu kizaa mama waliishi Nzega, na ndiyo
walionilea baada ya ndoa ya mama yangu na baba yangu kuvunjika.
Walinifundisha mambo mengi, kubwa likiwa ni kujiamini, pia kufanya mambo
yangu kwa bidii, uadilifu, umakini na kwa nidhamu ya hali ya juu. Bibi
yangu huyu hakusoma shule ya kizungu japokuwa alijifunza kusoma na
kuandika. Babu yangu alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya
kusoma Tabora School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na
alishiriki harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na
baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba
kila mtu anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba
ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya
wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo
alifanya juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama yangu aliishia
kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania
ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa
ajili ya mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki, naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai kwa
maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi
vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi
vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo
vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi
hiki.
Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu – vijijini
na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa
maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa
anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa
kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa
watumishi pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo
kwa wafanyabiashara, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao
zikitafunwa na wachache pale TRA, ama kulipa posho za bure kwa wabunge
na mawaziri kule Bungeni, kulipia mashangingi ya viongozi na watendaji,
kulipia tiketi za ndege daraja la kwanza kwa ajili ya safari za viongozi
na wataalamu wetu kwenda kujifunza kupambana na umaskini wakati
wakirudi wanauacha uzoefu uwanja wa ndege, ama kulipia semina, warsha na
makongamano ya wataalamu ya kuandika sera za MKUKUTA, MKURABITA na
kuandaa bajeti zisizotekelezwa kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda
kule kwa watani zangu, Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa ndugu zangu
kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali
itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali
haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya
kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote. Wanachohitaji wao
ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama
biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za
kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo,
wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa siku, wajue
wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala
kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote. Lakini wanaamini
kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna
tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi
wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya
baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu
kutoka miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa,
kwamba tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua
milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila
mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati
wowote ule kuanzia leo. Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza
bidii kwenye kazi akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora
kuliko jana yake, kuwa naye ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani
ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya
uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha
serikali yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo
yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa
vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye
uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua
mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Nyote mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu
la kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote;
tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa
tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa ili wakati muafaka ukifika muwape
taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa
kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa
uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha
wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale
inapolazimika baada ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za
kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na
wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba, anayeamini katika haki
ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa
watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora
za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama
wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na
wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote
wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao
kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea
kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani,
kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula,
kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi
ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za
hasara na faida za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu.
Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa
maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi
yetu.
Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya
watanzania walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo
wake, ndoto zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji
sahihi la watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa,
kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na
utayari wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo
mengi kwa kina: mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu,
uwepo wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa
kuchambua mambo, kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za
utekelezaji na kusimamia utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu, na
zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona
mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu
ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na
namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama
Taifa.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime
na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na
kuungwa mkono ama kutoungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa
jinsi yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye
jamii, dini yangu, ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa sifa na
uwezo wangu, kama mtanzania.
Watanzania tuna sifa moja kubwa; kwenye mambo ya msingi ya kitaifa,
tunakubaliana kuwa maslahi ya Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu
binafsi. Tudumishe utanzania wetu.
Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa
Jamhuri ya Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza,
viongozi waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye
matamanio yetu. Kizazi chetu cha kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza
Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za wazee na waasisi
wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala
wasiwasi, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta
tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo
na kesho: kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu
wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia
nchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi
kwa haraka na umakini wa hali ya juu.
Mimi ninaamini kwamba, kama hata mimi nimefika hapa, basi kila
mtanzania anaweza, na ana haki ya kufika hapa na kwenda mbele zaidi
yangu. Mafanikio siyo haki ya wachache, ni tunu ya Mwenyezimungu kwa
kila mtu. Ninaamini ni haki ya kila mtanzania kuota ndoto yake,
kuifanyia kazi na kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu
wa kutoa fursa kwa watu wake kuota ndoto zao na kufikia mafanikio bila
kukwama.
Na ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa, mbele yetu tuna
kazi ya ziada ya kufanya. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua;
uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa
kwenye kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama
wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka.
Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na
si yangu peke yangu, ni yetu sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule
Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama
siyo familia yangu.
- Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa
msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa
siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye
siyo babu yangu.
- Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja
wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo;
akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa
na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa
anafanya biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni,
hata kama yeye si mama yangu.
- Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini kwa
watani zangu warangi, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama
yeye si mwanangu.
- Bwana Kalumanzila ni mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye
huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la
Karume, akiuza anachukua kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na
kurudisha pesa ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama
tatu anayopata inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake. Akifukuzwa
barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na
analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali
iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana
Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si
mjomba wangu.
Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha
kimataifa cha maendeleo (Center for Global Development) alisema:
“…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi
masikini. Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu
kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka
mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi:
nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri.
Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu
kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Afrika.
Dk. Khamis Kigwangallah wakiigia katika chumba cha mkutano tayari kwa kuanza mkutano huo.
Dk Kigwangallah akitangaza nia yake ya kugombea urais wa Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania wakati alipokutana na waandishi wa habari, ambapo
amesema hajasukumwa na mtu yeyote ila ni yeye mwenyewe ameamua kwa moyo
wake.
Dk Kigwangallah akimtambulisha mke wake Dk Bayoum Awadh wakati wa mkutano huo.
Mzee Nasser Said Mussa, baba mzazi wa Dk. Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola.
Mzee Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dk Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola na watoto wake Sheila.
Mchungaji Patrick Saso akifanya maombi kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Sheikh Abubakary Mwita akiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Picha: Habari Mseto blog
Dk Kigwangalla amesema kutokea kuuza karanga na BigG
(bubble gum) mtaani mpaka kuwa Daktari, Mbunge na Kiongozi wa CCM Taifa
na kufikia na ndoto ya kutegemea kugombea Urais ina maana moja tu
kwamba sera za CCM zina tija kwa Taifa na wananchi wake na yeye ni mfano
wa kwanza mkubwa wa kuaminiwa kwamba sera hizo zinajali usawa kwa
wananchi kwani pamoja na kupitia yote aliyopitia bado anaweza kutuhubutu
kugombea Urais wa Tanzania kwa kukubaliwa na kuruhusiwa kikatiba na
chama chake CCM na kuruhusiwa kisheria na Sheria za Jamhuri ya Tanzania.
Sunday, 7 September 2014
DK KINGWANGALLA ATANGAZA NIA YA KUWANIA URAIS 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment