Mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amewaasa wanachama wa CCM katika Wilaya ya Bagamoyo, kuunganisha nguvu zao ili kulibakiza jimbo hilo mikononi mwa CCM.
Ridhiwani, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, aliyasema hayo mjini hapa jana baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa wilaya hiyo.
Alisema baada ya kampeni za kuwania uteuzi kumalizika, kazi iliyobaki sasa ni kushikana ili ushindi upatikane na hivyo kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na wabunge wa jimbo hilo waliotangulia.
“Wabunge waliotangulia walifanya kazi kubwa ya maendeleo katika jimbo letu, huduma za maji, afya, umeme, elimu na mengineyo," alisema.
Alisema endapo atashinda, ataendeleza mazuri yaliyofanywa na kushirikiana na wananchi ili kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka hivi sasa ikiwamo ya migogoro kati wakulima na wafugaji.
Pia aliwaelezea wananchi kuwa yeye ni mwanasiasa aliyetokea mbali tofauti na inavyoelezwa.
“Nimeanzia chipukizi nikiwa na miaka minne, nimekuwa Mjumbe wa Baraza la Chipukizi la Taifa kabla ya kuwa Mjumbe wa Nec, kwa hiyo situmii mgongo wa baba yangu,” alisisitiza Ridhiwani.
Ridhawani anakuwa mgombea mteule baada ya Kamati Kuu ya CCM, kumteua kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Chalinze kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo.
0 comments:
Post a Comment