JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA AJIRA KWA WALIMU WAPYA MWAKA 2013/14
Jumla ya Walimu wapya 36,021 ambao wamehitimu mwaka 2013 kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wataajiriwa rasmi na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri) ifikapo tarehe 01 Aprili 2014. Kati ya idadi hiyo walimu wa ngazi ya Cheti (Daraja III A) ambao hufundisha katika shule za Msingi ni 17,928 na walimu wa shule za sekondari ni 18,093 (wakiwemo 5,416 wa Stashahada na 12,677 wenye shahada).
Orodha rasmi ya walimu wapya ikionesha Halmashauri mbalimbali walikopangwa itatangazwa kwenye
tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI (www.pmoralg.go.tz) na ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (www.moe.go.tz) ifikapo tarehe 15 Machi, 2014.
Walimu wote wapya wanatakiwa kuripoti bila kukosa kwenye Halmashauri walikopangiwa ifikapo tarehe 01 Aprili, 2014 ili waanze kazi mara moja.
Inasisitizwa kwamba walimu waripoti tarehe hiyo ili taarifa zao za kiutumishi zifanyiwe kazi na Waajiri wao yaani Wakurugenzi ili kuwawezesha kupata mshahara mwezi Aprili 2014 na hivyo kuepuka ulimbikizaji wa mshahara kwa watumishi wapya wanaoanza ajira.
Mwalimu yoyote ambaye ataripoti baada ya tarehe 10 Aprili, 2014 bila sababu za msingi zinazokubalika kiutumishi atakuwa amepoteza nafasi hiyo.
Ikumbukwe kwamba Upangaji wa Walimu wapya kwenye Halmashauri umezingatia uwepo wa mahitaji ya walimu. Vile vile, fedha za kujikimu kwa muda wa siku saba na nauli ambazo zitalipwa kwa kila mwalimu atakayeripoti kulingana na viwango vilivyowekwa na Serikali zimetumwa kwenye Halmashauri walikopangwa walimu hao. Hivyo, kila mwalimu anatakiwa kwenda kuripoti katika Halmashauri alikopangwa.Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI haitafanya mabadiliko yoyote ya vituo vya kufanya kazi walimu wapya isipokuwa kwa utaratibu wa kawaida wa uhamisho baada ya mwalimu kutimiza vigezo na masharti ya uhamisho.
Ni vema ifahamike kuwa ajira zinazotangazwa ni za walimu wapya. Walimu ambao tayari ni watumishi umma waliokuwa vyuoni kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na hivi sasa wamehitimu mafunzo yao, wanatakiwa kurudi kwa waajiri wao na kuendelea na kazi.
IMETOLEWA NA
JUMANNE A. SAGINI
KATIBU MKUU
OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI
0 comments:
Post a Comment