Tuesday, 11 March 2014

CCM NA CHADEMA WATUNISHIANA MISULI MBELE YA MSAJILI

Filled under:



Viongozi  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambavyo vinashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga, Iringa, wametunishiana misuli mbele ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kila upande ukiushutumu mwingine kwa kujihusisha na matukio ya uvunjifu wa amani katika kampeni.
Habari kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo zinasema kuwa viongozi hao pia walalamikiana kuwa kumekuwa na tabia ya kuviziana, kufanyiana vurugu na kushusha bendera katika baadhi ya maeneo ya wapigakura.

Hata hivyo, Nyahoza akizungumza  jana alithibitisha kusikiliza malalamiko hayo, na kwamba alivitaka vyama hivyo kuachana na matumizi ya lugha zinazoudhi katika kampeni zao kwa maelezo kuwa kwa kufanya hivyo vinavuruga utashi wa wananchi  pamoja na kuhatarisha ukuaji wa demokrasia nchini.

Nyahoza alisema kuwa miongoni mwa mambo aliyosisitiza kwa viongozi wa vyama hivyo katika mkutano wao ni pamoja na kuachana na matumizi ya lugha za kuudhi katika kampeni pamoja na kuhakikisha kwamba hawasababishi matukio ya uvunjifu wa amani kutokana na tofauti zao za kiitikadi.

Alisema matumizi ya lugha za kuudhi katika kampeni hizo bado ni tatizo na kwamba vyama vinavyoshiriki haviweki ushindani sawa kwa wapiga kura wa jimbo la Kalenga ambao ndiyo wanaopaswa kuamua wataongozwa na nani kati ya mgombea wa Chadema, Grace Tendega; mgombea wa CCM, Godfrey Mgimwa na mgombea wa Chausta, Richard Minja, ambaye hajaanza kampeni hadi sasa.

“Lugha bado ni tatizo na siyo nzuri katika kampeni hizi na tunaviasa vyama vyenye ushindani kutotumia lugha za kuudhi ili kutoa uwanja sawa wa ushindani kwa wapiga kura kuamua wenyewe.

Ofisi yangu iko hapa kwa ajili ya kuangalia na kufuatilia vyama hivi vikuu vinavyochuana katika uchaguzi huu ambao utatupa picha halisi ya namna ya kufanya tathmini katika jimbo la Chalinze,” alisema Nyahoza.
Alisema mambo mengine ni pamoja na kuwahoji wagombea wa vyama vyote kuhusiana na mwenendo mzima wa kampeni hizo, huku ofisi hiyo ikihimiza vyama hivyo kuhubiri amani wakati wote watakapofanya mikutano ya kampeni katika jimbo la Kalenga.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya mkutano huo, vinaeleza kwamba viongozi wa CCM na Chadema walitaka kila upande uache kupiga na kujeruhi wafuasi ama wanachama wa  upande mwingine kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha amani na kusababisha umwagaji damu kabla ya kufanyika uchaguzi huo Jumapili ijayo.

Uchaguzi huo unaofanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Fedha, marehemu Dk. William Mgimwa, aliyefariki dunia Januari Mosi, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kloof Med-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini.

Hadi sasa matukio ya vurugu yaliyoripotiwa ni kutekwa na kujeruhiwa kwa Paroko wa Kanisa la Orthodox, Parokia ya Mtakatifu Basili Mkuu, jimbo la Kalenga pamoja na la kuchomwa kisu kifuani  Katibu wa Chadema, tawi la Ikuvilo katika Kata ya Ipamba, Richard Mawata.

Matukio mengine ni ya kung’olewa kwa mabango ya wagombea, baadhi ya wafuasi kujeruhiwa na kushushwa bendera za vyama hivyo.

NEC YAZUNGUMZIA MGOMBEA CHAUSTA
Wakati huo huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema suala la mgombea wa Chausta, Richard Minja, kutokufanya kampeni linamhusu yeye na chama chake.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba, alisema pamoja na NEC kumtambua kuwa ni mgombea kupitia Chausta, kila mtu anao uhuru wa kufanya kampeni kwa utaratibu anaoutaka, ili mradi havunji sheria na taratibu za NEC.

Mallaba alifafanua kwamba inawezekana mgombea huyo ameamua kufanya kampeni kwa siku moja, au kutokufanya kabisa jambo ambalo halimbani kisheria kwani hakuna sheria yoyote anayovunja.

0 comments:

Post a Comment