HARAKATI za
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) za kujiimarisha, jana
zilizidi kupata nguvu mpya baada ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani kujiunga nacho.
Makada
watatu wa CCM akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini
mwaka 2010, Dk. Rose Nkonyi, wamejiunga na CHADEMA.
Makada hao
walijiunga na CHADEMA jana na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama
hicho ngazi ya taifa, Freeman Mbowe, katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Mailimoja, ikiwa ni ziara ya Operesheni Movement For Change
(M4C) Pamoja Daima.
Waliojiunga
na CHADEMA mbali na Dk. Nkonyi ni Joseph Chakale, aliyekuwa mjumbe wa
Kamati ya Utekelezaji CCM ngazi ya wilaya na Hafidh Mudhihiri aliyekuwa
Katibu wa Vijana wa Tawi la Mailimoja.
Wakizungumza
katika mkutano huo makada hao walisema wameamua kuihama CCM baada ya
kubaini chama hicho hakina dhamira ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Waliongeza kuwa CCM hivi sasa imelemewa na tuhuma nyingi za ufisadi pamoja na kutumia vibaya rasilimali za wananchi.
Walisema
licha ya tuhuma hizo kukilemea chama hicho, viongozi wake wameshindwa
kuchukua hatua zinazostahili, jambo linalochangia ugumu wa maisha kwa
wananchi.
Mara baada
ya kuzungumza, makada hao walikabidhiwa kadi za CHADEMA na Mbowe
aliyewataka waendeleze harakati ili kuleta mabadiliko na ukombozi kwa
Watanzania.
Mbowe
aliwataka wananchi kuacha kumbeza mwanachama yeyote wa chama cha siasa
anayejiunga na chama akipendacho, kwakuwa kila mmoja huwa ana sababu za
msingi za kujiunga na chama kingine.
Mbowe pia
aliwataka wananchi kuiunga mkono CHADEMA katika harakati za maandalizi
ya Katiba Mpya na kusisitiza kuwa wanaunga mkono maoni ya rasimu ya
Katiba mpya.
Slaa: CCM wameganda
Katibu Mkuu
wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, akiwa mkoani Mwanza alisema viongozi wa
serikali ya CCM wana mawazo mgando ndiyo maana umaskini unazidi
kushamiri.
Alisema kutokana na mawazo hayo mgando kila kukicha wamekuwa wakipandisha gharama za bidhaa mbalimbali ikiwemo umeme.
Alibainisha
kuwa haoni sababu kwa serikali kupandisha bei za umeme wakati nchi ina
rasilimali nyingi ambazo kama zingetumika ipasavyo fedha nyingi
zingepatikana.
“Umeme si
jambo la anasa kwa binadamu, kwetu linaonekana ni anasa…..nishati hii
ilitakiwa kutolewa kwa gharama nafuu, viongozi wa CCM wana mawazo
mgando” alisema.
Alisema
mawazo mgando ya viongozi ndiyo yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada za
maendeleo ya wananchi huku wananchi wakibaki kuwa watazamaji wa
rasilimali zao badala ya wanufaikaji.
Dk. Slaa
alisema serikali imeshindwa kuendeleza vipaji vya vijana licha ya
kuwatumia kujipatia kura kila zinapofika nyakati za uchaguzi.
Alisema kuwa
CHADEMA itaendelea kuhakikisha daftari la wapiga kura linaboreshwa,
huku akiwataka Watanzania wakatae kuandikishwa na mabalozi wa nyumba
kumi ambao ni wa CCM.
Alisema kazi
hiyo ni lazima ifanywe na watendaji wa serikali kwa mujibu wa sheria za
nchi na si mabalozi hao ambao ni makada wa CCM.
“Mkiwaruhusu
mabalozi wawaandikishe mjue ni lazima udanganyifu utakuwepo kwa
kiwango kikubwa, hapa mtakosa haki ya kupiga kura,” alisema.
Alisema CCM
wanataka kuitumia fursa hiyo kuwanyima watu haki ya kuwachagua viongozi
wanaowapenda, hasa katika kipindi hiki ambacho upinzani una nguvu.
Aliwataka
Watanzania wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu ili wachague viongozi
wanaowataka.
Dk. Slaa pia
amewataka wananchi wawe makini katika maamuzi yao ili viongozi
watakaowachagua wawasaidie kuliendeleza gurudumu la maendeleo yao.
Alisema
mwaka 2015 nchi inahitaji kupatikana kwa viongozi bora, wawajibikaji
zaidi, tofauti na hawa wa CCM wanaoendekeza matumbo yao na jamaa walio
karibu nao.
Aliwataka viongozi wa CHADEMA kuhakikisha wanakuwa wabunifu katika harakati za mapambano ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Kuhusu
madini yanayopatikana hapa, jambo hilo bado limeonekana ni balaa au
hasara kwa Watanzania ambao hawanufaiki kama walivyo wageni.
Amesema kuwa
kama serikali ingekuwa makini, ingekuwa na viwanda vya kuchakata madini
ambavyo vingetoa ajira kwa vijana na kukuza pato la taifa.
“Fedha zote zinapelekwa nje ya nchi, tukiingia madarakani tutatumia vizuri madini kwa manufaa ya watu wote,” alisema.
Alisema CHADEMA wanajua mahitaji ya wananchi na vijana ambao wana tatizo kubwa la ajira.
Alibainisha kuwa CHADEMA inataka kuona vijana wanapata fursa za ajira zitakazowasaidia kuondoa umaskini walionao.
Serikali ifufue viwanda vya nguo ili kuleta nafuu kwa wakulima ambao wanalima pamba na malighafi mbalimbali.
Alibainisha kuwa uwepo wa viwanda hivyo vitasaidia pamba inayozalishwaji nchini kupata soko la uhakika.
Aliwataka
wabunge wa Bunge la Katiba wakiingia kwenye Bunge hilo watumie busara na
hekima katika majadiliano ili Tanzania iwe na Katiba bora na imara.
“Hatuhitaji
katiba yenye viraka viraka au milengo ya kisiasa, walete Katiba yenye
kujali matakwa ya wananchi waliowapa fursa ya kuingia bungeni,” alisema.
0 comments:
Post a Comment