KASHFA ya ukahaba iliyokuwa inakikabili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
pamoja na maandamano na migomo, vimekuwa vikimnyima usingizi Makamu Mkuu
wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula.
Profesa Kikula alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza
na walimu pamoja na wanafunzi wa chuo hicho kwenye hafla ya kukabidhi
makombe pamoja na medali walizoshinda kwenye mashindano ya SHIMMUTA na
TUSA.
Alisema kashfa hiyo ilimnyima usingizi kiasi kwamba ilifika mahali
akajiuliza anafanya nini katika chuo hicho, ndipo alipoamua kufanya
uchunguzi wake binafsi.
“Kwa kweli ile kashfa ya ukahaba wa wanafunzi iliyokuwa inasemwa hapa
chuoni ilikuwa inaninyima usingizi… ilifika wakati nikajiuliza sasa
nafanya nini hapa?” alisema Profesa Kikula.
Profesa Kikula alisema aliamua kufanya uchunguzi ili kujua kama
habari zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na chuo hicho
ni za kweli, lakini alibaini zilikuwa ni njama za baadhi ya watu
waliotaka kukichafua chuo kwa maslahi binafsi.
Alisema katika uchunguzi wake alibaini kuwa kuna baadhi ya wasichana
wanaojiuza mjini hapa ambao walikuwa wanajiita wanafunzi wa UDOM wakati
si kweli.
Mbali ya kashfa hiyo ya ukahaba, mambo mengine yaliyokuwa yanamnyima
usingizi kuwa ni pamoja na maandamano, migomo na migogoro iliyokuwa
ikiendelea chuoni hapo.
“Miaka mitatu iliyopita UDOM ilichafuka kiasi kwamba wanafunzi
waliokuwa wanahitimu walishindwa kuajiriwa mahali popote kwa sababu
walionekana wakorofi na wasiokuwa na maadili,” alisema.
Hata hivyo, alisema hivi sasa hali imetulia na wanafunzi wanaotoka
chuoni hapo wamekipa sifa nzuri chuo hicho kwa uhodari wao kazini.
0 comments:
Post a Comment