Raia wawili wa Ufaransa wameuawa na
kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba
yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini,
Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza
kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.
DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari
vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima
hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu
wa kushoto wa mmoja wa watu hao.
Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni
Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi
kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa
amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa
Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba
kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza
kuishi eneo hilo.
DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia
watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja
anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani
ya kisima kilichomo ndani ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na
siyo ya siku moja,” alisema DCI Ilembo.
Gazeti hili limefanikiwa kufika katika eneo la
nyumba hiyo na kukuta askari Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku
harufu kali ikitoka katika shimo la kisima.
Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.
Mlinzi mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa
akilinda nyumba hiyo baada ya kuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa
amesema alikabidhiwa kazi ya ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na
hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.
“Kazi yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na
mwajiri, sijui lolote, mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na
watu kabla au la, sina la kusema na sijui nianzie wapi,” alisema Omar.
Sheha wa Matemwe Kusini
Sheha wa Shehia ya Matemwe Kusini, Denge Khamis Silima
aliyelizungumzia suala hilo kwa niaba ya Sheha wa Matemwe Kaskazini,
aliliambia gazeti hili kuwa taarifa za kutoweka kwa wazungu hao zilianza
kuenea kuanzia Desemba 27 mwaka jana.
Denge alisema alianza kupata taarifa za awali
kutoka kwa mjumbe mmoja wa Shehia aitwaye Mkadam Tabu Vuia kwamba mlango
wa nyumba ya wazungu hao ulikuwa wazi kwa muda mrefu na harufu kali
ikitoka na inzi wakubwa wametanda katika eneo hilo.
“Nimeshiriki katika kazi ya kuchimbua kisima,
askari wametoa mfupa wa mguu na unyayo unaoaminika kuwa ni wa mtu,
ingawa tuliikuta nyumba ikiwa haikuvunjwa milango,” alisema.
Alisema waliingia ndani ya nyumba hiyo kupitia
dirishani wakakuta mbwa wa wazungu hao, Allan naye amekufa na kwamba kwa
sasa wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa polisi.
Sheha huyo wa Shehia ya Matemwe Kusini alisema
mazingira waliyoyakuta ndani ya nyumba hiyo yameonyesha kuwa haikuhamwa
kwa muda mrefu na kama kwamba wanatarajia kurejea wakati wowote.
Alisema baada ya kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi
wa Wilaya, askari polisi walifika katika eneo hilo na kazi ya kuchimba
kisima ilianza baada ya kubaini harufu kali ilikuwa inatoka kisimani.
0 comments:
Post a Comment