Saturday, 1 February 2014

JOHN MALECELA ATOA TAMKO KALI DHIDI YA LOWASA

Filled under:



Tamko la Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, dhidi ya mwenzake aliyejiuzulu katika wadhifa huo, Edward Lowassa, wote wakiwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), limetishia kuigawa nchi.
Mgawanyiko huo unatokana na makundi ya wana-CCM kulumbana na kupinga matamko ya kushutumiana kwenye mijadala mbalimbali.

Wakitoa maoni yao watu wa kada tofauti wametoa kauli zinazotofautiana katika ama kumpongeza au kumkosoa Malecela.

Waliomuunga mkono Malecela, walielezea hisia zao kwamba karipio kali dhidi ya Lowassa ni moja ya nyenzo imara kwa CCM hususani Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, kutafuta suluhu itakayokiokoa chama hicho dhidi ya mpasuko wakati kikijipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwakani.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema; "nadhani tutafika mahala utatokea mgawanyiko na kuleta mpasuko ndani ya CCM.”

Alionya kuwa kama Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, hatafanya juhudi za kuwaweka pamoja wanachama wanaotofautiana kimtazamo kuna hatari mwaka ujao kikapoteza nguvu ya kuendesha kampeni za uchaguzi mkuu kutokana na majeraha haya.

Alisema mgawanyiko ndani ya chama hicho ulianza baada ya mawaziri walioitwa mizigo kuendelea na kazi hiyo, hivyo kuonekana mazungumzo kwa kutumia vikao hayaleti ufumbuzi.

"Kutokana na hili kuna ugumu wa kumsikiliza Mwenyekiti, inawezekana asiaminiwe hata akitoa tamko,” alisema na kuishauri CCM itafute njia ya kutibu.
Alisema mitafaruku ya aina hiyo inaibuka katika vyama vyote vya siasa, jambo linaloweza kuhatarisha amani ya nchi.

Alimshauri Rais Kikwete, kutumia maadhimisho ya miaka 37 ya CCM, kujenga mwafaka mpya na kuweka mazingira bora ya kuaminiana.

"Kila mara ninapopata nafasi navihimiza vyama vya siasa vijitahidi kujenga mshikamano na maelewano, tofauti za watu wanaogombea vyeo itasababisha wananchi kuyumbishwa bila sababu ya msingi,"alisisitiza.

Mhadhiri wa siasa za uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye hakutaka jina litajwe alisema malumbano hayo ambayo yanaendelea ni mchezo mchafu usio na manufaa kwa taifa.
Alisema wanachokifanya si kuboresha jambo lolote na matokeo yake ni kugawa makundi ndani ya CCM.

Alionya jambo hilo linaweza kuleta hatari na kuwagawa Watanzania badala ya kulumbana katika masuala ya msingi ikiwamo changamoto za umeme, miundombinu na elimu na masuala ya kuijenga nchi.

“Endapo vitendo vya rushwa, mgawanyiko na malumbano vitaendelea, CCM itameguka na kuvuruga utulivu nchini,”alionya

DK BANA
Mwanazuoni mwingine wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema maoni ya Malecela ni mazuri lakini yamechelewa kutolewa na kuhoji ni kwanini asimfute Lowassa kumueleza ukweli mpaka akamshambulie kupitia vyombo vya habari.

Alimshauri kuwa kiongozi mstaafu aliyewahi kutumikia taifa kwa nyadhifa mbalimbali alitakiwa kutumia hekima na busara bila kutumia vyombo vya habari kwani wote walishakuwa mawaziri wakuu na ni makada wanaoheshimika ndani ya CCM.

"Hao wazee wastaafu huwa wanataratibu zao zenye hekima nadhani Malecela ana maoni mazuri lakini kachelewa kuyatoa," alisema Dk Bana, mhadhiri wa sayansi za siasa.
Aliongeza kuwa Lowassa hajavunja sheria za nchi na kama amekiuka utaratibu wa chama walitakiwa wamfahamishe lakini matokeo yake hayo hayafuatwi.

"Hapo kuna jambo limejificha sidhani kama Lowassa ni mzito kupita chama labda wanamuogopa kumueleza," alisema.

SUMAYE
Mwanasiasa mwingine aliyezungumzia mgogoro huo ni Waziri Mkuu mstaafu, Federick Sumaye, aliyempongeza Mzee Malecela kwa hatua ya kukemea hadharani vitendo vya rushwa.

"Namuunga mkono Mzee Malecela kwa msimamo wake huo kwani unakwenda sawa na kile ninachokikemea siku zote watu wanaotafuta madaraka kwa hila ya rushwa," alisema Sumaye.

Alieleza kuwa kilichobainika kimewafumbia macho wananchi, kiasi ambacho sasa wanatambua nani anahusika na vitendo hivyo vibaya.

Aliongeza kwamba uongozi wa nchi hautatokana na nguvu ya fedha ya badala yake wananchi wapewe nafasi ya kuchagua kutokana na uwezo na siyo uwezo wa utendaji wa kazi.

"Ninachoomba wananchi waone na wasimamie katika ukweli na haki, tusipopambana hali ya chama itakuwa mbaya," aliongeza kusema.

Aidha, Sumaye alisema CCM kupitia vyombo vyake na vikao kufanya kazi ya kudhibiti na kuangalia njia ya kuwaengua watu wa aina hiyo.

LUGOLA
Kwa upande wake mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema hakuna malumbano ya kupasua chama kwani kina mizizi iliyokomaa.
Alisema kwa sasa kila mtu anaibuka na mtazamo wake pamoja na mawazo yake lakini wanaendelea kuwa wamoja.

Wiki hii Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ulimshambulia Lowassa kuwa anatumia fedha kutafuta urais na kuwataka viongozi wanaohitaji fedha waende kwa mgombea huyo aliyeonyesha nia ya kuwa Rais uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Juzi Malecela, alimpinga Lowassa hadharani kuwa anausaka urais kwa kutumia fedha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment