Zaidi ya watu 10 wamenusurika kufa maji baada ya kujitosa ndani
ya Mto Songwe, wakihofia kukamatwa wakati wakivusha sukari ya magendo
kutoka nchi jirani ya Malawi.
Walikuwa wanahofia kukamatwa na askari polisi
waliokuwa wameongozana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati
alipotembelea mpaka wa Tanzania na Malawi wa Kasumulu, wilayani Kyela.
Katika tukio hilo, watu hao waliamua kuitupa majini, sukari na baiskeli moja waliyokuwa wakiitumia.
Baadaye wao wenyewe walijitosa mtoni na kuanza kupiga mbizi.
Tukio hilo lilitokea juzi baada ya Naibu Waziri
Nchemba na msafara wake, kuwasili katika kivuko cha Timotheo, umbali wa
kilometa tatu kutoka ulipo mpaka rasmi wa Kasumulu.
Vijana hao walikuwa wanatumia mtumbwi wa jadi, kuvusha sukari hiyo kutoka Malawi na kuiingiza nchini.
Nchemba alitembelea vivuko viwili kati ya 32
ambavyo ni njia za panya zinazotumika katika kuvusha bidhaa za magendo
na hivyo kulikosesha taifa mapato.
Baada ya kuvuka mto, baadhi ya vijana walitimua
mbio na wengine walioshindwa kuogelea, waliokolewa na kutolewa ndani ya
maji kwa tabu.
Wakizungumza baada ya kuokolewa, vijana hao
walisema wanafanya biashara hiyo ya magendo kwa lengo la kupata fedha za
kujikimu na kuwasomesha watoto wao.
“Tunashindwa kutumia mpaka halali kuingiza sukari
hiyo nchini kwa sababu bidhaa hiyo hairuhusiwi kisheria kuingizwa
nchini. Pia hatuna uwezo wa kulipa ushuru mkubwa na sisi mitaji yetu ni
midogo, wengi wetu tuna mitaji ya kuanzia kilo 20 hadi 100,”alisema
mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Lugano.
Alisema pia baadhi ya vijana wanaovusha sukari
hiyo, hawana mitaji ya kuendeshea biashara hiyo na kwamba wanatumiwa na
wafanyabiashara wakubwa kuingiza sukari kwa magendo na kulipwa ujira
kidogo unaowawezesha kujikimu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya ya Kyela, Magreth Malenga alisema changamoto kubwa katika
kupambana na biashara ya magendo ya sukari ni uhaba wa watumishi na
vitendea kazi.
Pia kukosekana kwa sukari ya Tanzania katika maeneo mengi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Alisema wakati mwingine hushindwa kuweka mkazo wa
kuzuia sukari hiyo kuingizwa nchini kutokana na hali halisi kwamba
wananchi hawana sukari mbadala kwa sababu sukari ya Tanzania haipatikani
kirahisi.
Kwa upande wake, Nchemba alisema amejionea ukubwa wa tatizo na kwamba Serikali italifanyia kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Pia aliwataka vijana hao, kujiandaa kisaikolojia,
ili kufanya biashara kwa njia halali na zinazokubalika badala ya njia
hiyo inayoweza kusababisha matatizo.
0 comments:
Post a Comment