Mwanamke mmoja raia wa Ethiopia anayesema kuwa
alibakwa na genge la watu nchini Sudan amehukumiwa kifungo cha mwezi
mmoja jela kwa kosa la kufanya 'kitendo kichafu'.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 18 alikuwa na mimba ya miezi mitatu wakati alipovamiwa na genge la wanaume na kubakwa.
Alikamatwa baada ya kanda ya video iliyoonyesha akibakwa iliposambazwa kupitia kwa mitandao ya kijamii.
Wanaume watatu waliokiri kufanya mapenzi na mwanamke huyo na wawili waliosambaza kanda hiyo wataadhibiwa kwa kuchapwa mijeledi.
Kwa mujibu wa shirika moja la kutetea haki za
wanawake (Strategic Initiative for Women) katika upembe wa Afrika
(SIHA),watatu hao watapokea viboko miamoja kila mmoja kama adhabu ya
kosa la zina wakati wawili wakiadhibiwa mijeledi 40 kwa kusambaza kanda
yenye picha chafu.
Mwanamke huyo alifungwa jela mwezi mmoja lakini adhabu hiyo ilifutiliwa mbali kwa sababu ya ujauzito wake.
Pia alitozwa faini ya dola 880.
Kadhalika alikabiliwa na makosa ya zina pamoja
na ukahaba, ambayo adhabu yake ni kifo kwa kupigwa mawe nchini Sudan.
Lakini hakupata adhabu hiyo kwani alishawishi mahakama kuwa ametalakiana
na mumewe.
Inaarifiwa mwanamke huyo alikuwa anatafuta
nyumba ya kupangisha wakati alipohadaiwa na kuingizwa ndani ya nyumba
moja ambapo wanaume hao walimbaka mjini Omdurman.
Mwanamke huyo huenda akarejeshwa nchini Ethiopia.
Shirika hilo limelaani adahabu dhidi ya mwanamke huyo likisema kuwa litawazuia wanawake kuripoti visa vya ubakaji.
0 comments:
Post a Comment