Kadiri siku zinavyosogelea uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, ndivyo mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
unavyozidi, kutokana na kuwapo kwa makundi mawili yanayojipanga
kusimamisha wagombea na ambayo yameanza kuendesha kampeni kuchafuana.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa makundi
hayo ni yale yanayomsaidia aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Andrew Chenge na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambao wametajwa
kutaka kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, wakati Chenge akiwa hayuko tayari
kuthibitisha nia yake hiyo, Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala
hilo. Lakini habari zinasema vigogo hao wameshajipanga kwa ajili ya mbio
hizo za uchaguzi na sasa wanatafuta watu wa kuwasaidia.
Makundi hayo yalianza wakati wa kikao cha ndani
cha CCM kilichofanyika mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais
Jakaya Kikwete, ambako habari zilisema, baada ya chama kumteua Pandu
Ameir Kificho kuwania nafasi ya mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba,
mmoja wa wajumbe wa kikao hicho walimpendekeza Chenge kuwa mwenyekiti wa
kudumu wa bunge hilo.
“Hapo ndipo mgogoro ulipoanza. Kwanza tulimkubali
Kificho ili kupunguza wingu la ushindani kwenye uchaguzi wa mwenyekiti
wa kudumu. Lakini wajumbe tulimkataa Chenge kwa hoja nzito na mwenyekiti
alikubali na kuamua kuwa watu wakagombee bungeni.”
Tuhuma dhidi ya Chenge
Baadhi ya wabunge wa CCM wamesema ni ukweli ulio
wazi kwamba Sitta na Chenge ndio wanaofaa kuwania nafasi hiyo, lakini
mchuano utakuwa mkali kutokana na kila mmoja kuwa na ushawishi wa aina
yake kwa wajumbe ambao ndio watakaopiga kura kumchagua mwenyekiti.
“Wakati wa kuapa, wajumbe watatakiwa kushika
Biblia au Qur’an. Ila tusema ukweli, unawezaje kufanya kiapo cha utii
mbele ya mwenyekiti ambaye uadilifu wake unatia shaka? Alihoji mmoja wa
wajumbe wanaomuungano mkono Sitta.
Mjumbe mwingine alisema Chenge hazuiwi kugombea,
lakini ajiandae kujibu maswali makuu matatu, moja likihoji uadilifu wake
wakati kuna mikataba mingi ya wawekezaji kwenye kampuni za madini
iliyoshuhudiwa na yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni mibovu.
“Pia tutamtaka aeleze kwa nini alikubali Uenyekiti
wa Kamati ya Bajeti ya Bunge la Jamhuri kwa uteuzi wa Spika, wakati
kanuni zinasema wenyeviti wachaguliwe na wabunge wenyewe,” alisema
mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Kauli ya Chenge
Chenge mwenyewe amepuuza tuhuma hizo akisema kuwa ni za watu wasiopenda kuelewa.Hayo yote na mengi zaidi nimeyasikia ndiyo maana nimeamua
kuondoka Dodoma. Siko Dodoma nitarudi Jumatatu,” alisema Chenge na
kuendelea;
“Lakini ndugu yangu, mi naona hakuna haja ya
kulumbana na watu ambao hawataki kuelewa. Kama watu wanatuhumu, lakini
hawana kielelezo cha kwenda nacho mahakamani, wanaambiwa kwa ushahidi
kuwa tuhuma zao hazina msingi na hawataki kusikia, unadhani
tutawafanyaje zaidi ya kuwaacha tu?”
Alipotakiwa kuthibitisha kuwa kweli ana mpango wa kugombea nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alijibu;
“Chama kina utaratibu wake na mipango yake. Ni
taasisi inayopaswa kuheshimiwa, kwa nini tulumbane leo wakati chenyewe
kina msimamo wake juu ya hilo?”
Alipoulizwa tena kueleza namna anavyojiandaa
kujibu maswali matatu magumu yanayoandaliwa na wapinzani wake, endapo
atasimama kunadi sera zake akitakiwa kugombea nafasi hiyo alijibu;
“…Bwana! Chenge ni huyo huyo, chaguzi ni hizo hizo ambazo ameshinda mara kadhaa na nchi hii ni yetu sote.”
Sitta
Sitta hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo,
lakini mmoja wa wanaomuunga mkono ambaye hakutaka jina lake litajwe,
amesema hawana shaka kwamba akisimama na Chenge kwa kura za haki,
atapita.
Tayari kumeripotiwa taarifa za rushwa kwenye mbio
hizo za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Hata hivyo,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameonya vitendo hivyo na kuzitaka jumuiya za
CCM kuwa macho dhidi ya suala hilo.
Pinda alitoa karipio hilo jana alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi mjini Dodoma.
Alisema viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa
siyo viongozi bora na kuhoji, “Hivi mtu anayetumia fedha kuingia
madarakani akipata madaraka fedha hizo atazirudishaje?”
Pinda ametaka jumuiya hiyo kuwa mstari wa mbele
kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndani ya chama kwa misingi ya maadili,
kwani wanaomwaga fedha ili kupata uongozi ndani ya chama wanawavuruga na
hiyo siyo njia ya kukijenga chama
Pinda aliwaasa wanachama wa CCM waache kupanga nani agombee na
nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya
chama hicho.
“Tunahitaji kupata viongozi kwa kuzingatia umoja
wetu na mshikamano miongoni mwa wanachama. CCM ikiwa imara itaunda
Serikali imara. Chama kikiwa dhaifu ni wazi kuwa hata Serikali yake nayo
itakuwa dhaifu,” alisema.
.
0 comments:
Post a Comment