Mbunge wa Bahi(CCM), Omar Badwel ameingia katika kashfa baada ya
Kamati ya Uhakiki wa Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kubaini
matumizi mabaya ya fedha hizo.
Kamati hiyo iliyoundwa na Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, ilibaini kuwa fedha hizo zilitumika
kinyume cha lengo la mfuko huo na pia taratibu za ununuzi
hazikuzingatiwa.
Kuundwa kwa kamati hiyo yenye wajumbe watano,
kulitokana na kuibuliwa kwa hoja ya ufisadi na Diwani wa Kata ya
Lamaiti, Donald Mejitii mwishoni mwa mwaka jana.
Mejitii, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CCM Mko
wa Dodoma alisema fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ununuzi na
usambazaji wa majembe ya kukokotwa na ng’ombe.
Akizungumzia tuhuma hizo, Badwel alisema
inawezekana kuwa kuna tatizo katika mfuko huo lakini akadai ripoti hiyo
ina ukweli na uongo pia.
“Katika ripoti hiyo, sijaona sehemu ambayo mimi
nilitoa majembe kwani katika mzunguko huu na mimi nilipeleka majembe 58
kwa ajili ya wananchi wangu. Nadhani mnyonge mnyongeni lakini haki yake
mpeni,” alisema.
Akisoma taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Bahi jana, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Julius Chitojo ambaye pia ni Diwani wa Zanka, alisema wamebaini
wananchi wamedanganywa kwa kuuziwa majembe hayo kwa madai kuwa yana
chapa ya Zimbabwe.
Pia, ilibaini kuwa majembe yaliuzwa kwa wananchi
kwa Sh110,000 wakati makubaliano ya Kamati ya Mfuko wa Jimbo yalikuwa ni
Sh85,000.
“Pia tumebaini kuwa makusanyo ya fedha kutokana na
mauzo ya majembe hayo hayajarudi halmashauri ili wananchi walio wengi
waweze kunufaika na mfuko huo wa jimbo badala yake fedha hizi
zimechukuliwa na Said Kayumbo kwa maelekezo kuwa anampelekea Mbunge
Badwel,” alidai Chitojo.
Chitojo alisema baadhi ya wananchi wamepata mgawo
wa majembe ya bure wakati wengine wameuziwa na pia fedha za vikundi
ziliingizwa katika akaunti ya Jumuiya ya Akiba na Maendeleo ya Bahi
(Basada) kinyume na utaratibu.
Kuhusu madai hayo Badwel alisema alitoa orodha ya
vijiji ambavyo alitoa majembe yaliyotolewa kwa mfuko wa jimbo na mengine
ambayo sio ya mfuko lakini hayakuainishwa katika ripoti hiyo.
“Nilipoulizwa kuhusu fedha zilizotolewa kwa
vikundi nilisema fedha zote zimetolewa na zimefika katika vikundi,
nashangaa hapa kwenye taarifa haijaelezwa, vitu nilivyovisema
havijatolewa, vitu vimepangwa na kamati,” alisema Badwel.
Aidha, Chitojo alidai kwamba Mbunge huyo alihujumu mradi wa
kusafisha kisima cha maji katika Kijiji cha Chibelela kwa kuchukua fedha
za mchango kwa kazi hiyo katika kipindi cha Januari na Februari 2013 na
hazikuwa zimerejeshwa mpaka kufikia Oktoba 30, 2013 wakati baraza
lilipounda Kamati ya Uhakiki.
Akizungumzia madai hayo Badwel alisema alitoa Sh2 milioni kwa ajili ya mradi huo na wananchi wa Bahi walichangia Sh1.7 milioni.
“Hajiuzulu mtu hapa. Kama kuna mtu ana matarajio
ya ubunge afute maana kuna watu wanaota tu ubunge, watu hawatoki hivyo.
Mjinga ni kwenda tu lakini wakati wa kurudi siyo mjinga yaliyotokea ni
ya kupandikizwa tu,” alisema Badwel.
Katika ripoti yake, Chitojo alipendekeza Baraza
kuchukua hatua stahiki dhidi ya mbunge huyo pamoja na kumtaka kurejesha
fedha zote anazodaiwa kupokea kinyume na utaratibu.
Pia kamati hiyo imeagiza kuadhibiwa kwa baadhi ya
maofisa wa Basada. Chitojo alisema baadhi ya maofisa wa Basada
wanatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutoa risiti ambazo si za
ununuzi wa majembe na pia kukopesha fedha ambazo zilikuwa zinatakiwa
kuwa za ruzuku.
Baada ya kuwasilishwa ripoti hiyo, kulitokea
mvutano miongoni mwa madiwani baadhi wakidai kuwa wanataka kujua kanuni
na taratibu za fedha za mfuko wa jimbo na wengine walitaka ripoti hiyo
ipelekwe kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili
uchunguzi wa kina ufanyike kuwabaini wote waliohusika na kuchukuliwa
hatua.
0 comments:
Post a Comment