Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi inayomkabili
aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mwenye namba G.
2573 Pacificus Cleophase jana ilianza kusikilizwa kwa mara ya kwanza
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.
Wakati kesi hiyo ikisikilizwa, jijini Dar es
Salaam, mshtakiwa mmoja kati ya 11 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya
kukusudia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk
Sengondo Mvungi, Longishu Losingo (29) amelalamika kuwa wanalishwa
mchuzi wa maharage gerezani.
Kesi hiyo ya Mwangosi inasikilizwa na Jaji Mfawidhi, Mary Shangali.
Wakili wa Serikali, Adolf Maganda alidai kuwa
mtuhumiwa Cleophase ambaye alikuwa askari polisi mkoani Iringa alifanya
mauaji hayo Septemba 2 mwaka 2012 katika eneo la Nyololo, wilayani
Mufindi.
“Mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati alipokuwa
akiwaamuru wafuasi wa Chadema kuondoka katika eneo la tukio walipopanga
kufanyia mkutano,” alidai.
Maganda alidai kuwa katika tukio hilo, mtuhumiwa alifyatua risasi na kumpiga marehemu.
Wakili huyo alidai kuwa wafuasi wa Chadema
walifika katika eneo hilo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano ambao katibu
mkuu wa chama hicho alikuwa anatarajia kuhutubia.
Alisema mkutano huo ulikuwa ufanyike licha ya polisi kuwaandikia Chadema ikiwataka wauahirishe ili kupisha zoezi la sensa.
Aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kuzuiwa
kufanya mkutano, wafuasi wa chama hicho walianza kurusha mawe na
kuwaumiza baadhi ya askari polisi, hatua iliyowalazimisha kuwatawanya
kwa mabomu ya machozi na kwamba hatua hiyo ilikuja baada ya kuwasihi
kutokufanya mkutano huo.
Maganda alidai kuwa mshtakiwa akiwa na bunduki
alikwenda katika eneo la tukio alilokuwa marehemu na kufyatua risasi na
kumpiga marehemu ambaye alikufa papohapo. Alidai kuwa taarifa ya daktari
inaonyesha kuwa kifo cha Mwangosi kilisababishwa na kupatwa na majeraha
yaliyotokana na mlipuko mkali.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, katika hali isiyokuwa
ya kawaida askari polisi walimkamata Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi
wa Habari wa Mkoa wa Iringa, Frank Leonard kwa madai kuwa alipiga picha
mahakamani.
Baada ya kukamatwa, Leonard ambaye pia ni
mwandishi wa Gazeti la Habari Leo na Daily News alifikishwa katika Kituo
cha Polisi cha Kati na kuhojiwa kwa muda kabla ya kuachiwa.
0 comments:
Post a Comment