Thursday, 13 February 2014

NAPE ATOFAUTIANA KAULI NA WARIOBA

Filled under:


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema Bunge Maalumu la Katiba, litatekeleza majukumu yake kwa kufuata Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na si mawazo ya mtu yeyote.

Kauli hiyo ya Nape imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kusema kuwa litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge hilo kubadili hoja ya msingi iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba, akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuifanyia marekebisho
Warioba alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kuhusu tafakuri na maridhiano kuelekea katika Katiba Mpya.
Alisema kama Bunge Maalumu la Katiba likipewa jukumu la kuandika Katiba linaweza kubadili mambo mengi, lakini kama Katiba itakuwa imeandaliwa na chombo kingine, Bunge hilo linatakiwa kutobadili hoja za msingi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nape alisema: “Mchakato wote wa Katiba Mpya unasimamiwa na sheria na sio maneno ya Warioba. Sheria inazungumzia haki, wajibu na mamlaka ya Bunge hilo, hivyo inawezekana kabisa kuboreshwa na hata kubadilishwa kwa hoja.”
Nape alisema kulingana na sheria hiyo, Bunge hilo lina mamlaka ya kufanya jambo lolote katika Rasimu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuifanyia maboresho kadri itakavyoonekana kuwa inafaa.
“Bunge haliwezi kutishwa na mtu yeyote kwa sababu lipo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi. Ndiyo maana baada ya Bunge hilo kwisha wananchi watapiga kura ya maoni,” alisema.
Akitolea ufafanuzi kauli ya Jaji Warioba kwamba Bunge hilo lifanye maboresho na si kubadili hoja za msingi, Nape alisema: “Maboresho maana yake ni kubadili. Ukiwa na nyumba ya vyumba vinne na kuiboresha kwa kuweka chumba kimoja si umeibadili?”
Alisema Bunge hilo linatakiwa lisiingiliwe katika uamuzi wake.

0 comments:

Post a Comment