CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka serikali ya Rais Jakaya
Kikwete kutoa majibu ya maswali yaliyoulizwa na mwandishi wa gazeti la
Daily Mail la nchini Uingereza kwa vielelezo, badala ya kulalamika kuwa
tuhuma hizo zina lengo la kuichafua nchi.
Wakati
CHADEMA ikiwa na msimamo huo Umoja wa Wabunge wa Kuhifadhi Mazingira ya
Ulinzi wa Tembo na Faru, umetaka uchunguzi ufanywe dhidi ya watu
wanaodaiwa kuwa karibu na mamlaka za serikali huku wanatuhumiwa
kujihusisha na ujangili ili kubaini ukweli.
Msimamo wa
CHADEMA ulitolewa jana jijini Dar es Saalaam na Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa wakati akizungumza na
waandishi wa habari.
Msigwa
alisema baada ya gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza kuripoti
ugumu wa kukabiliana na ujangili nchini kutokana na wahusika kuwa karibu
na mamlaka ya serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalaundu, alisema tuhuma hizo zimelenga kuichafua Tanzania.
“Waziri
Nyalandu anasahau kuwa Tanzania imeshajichafua katika Jumuiya za
Kimataifa baada ya kushindwa kulinda rasilimali zake kutokana na matendo
ya ujangili yanayoshika kasi kila siku.
“Nyalandu
atuambie amechukua hatua gani kuwalinda wanyama hao wakiwa hai zaidi ya
kukamata pembe za ndovu na faru waliokufa?.. je, hakuona taarifa
iliyorushwa na kituo cha ITV cha Uingereza namna wachunguzi wao walivyo
rekodi namna pembe hizo zinavyopatikana na watu wanaohusika?” alihoji
Mchungaji Msigwa.
Alisema
pamoja na serikali kuona jambo hilo ni dogo, lakini wanasahau kuwa
Jumuiya ya Kimataifa ipo makini katika kulinda viumbe hai vilivyo katika
hatari ya kupotea.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Kuwalinda Tembo na Faru,
Dk. Athuman Mfutakamba, ambaye aliongea muda mfupi baada ya Msigwa
kukutana na waandishi wa habari, alisema licha ya kutaka uchunguzi
lakini pia wanalaani upotoshaji uliofanywa na gazeti hilo kwa lengo la
kuichafua Tanzania.
Kauli hiyo
ilitokana na swali kutoka kwa mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua
kama umoja wao una lengo la kutaka uchunguzi ufanyike juu ya tuhuma hizo
na kwanini wasiiachie Ikulu ijisemee juu ya watu wanaodaiwa kuwa karibu
na Rais Kikwete kujihusisha na ujangili.
Akijibu
swali hilo alisema wao kama walinda mazingira na watetezi wa faru na
tembo, wangependa uchunguzi ufanyike na wahusika wajulikane badala ya
tuhuma za upande mmoja kufanyiwa kazi na kusambazwa kwa jamii.
“Tumeshtushwa
na gazeti moja la kihafidhina la Uingereza lililochapishwa Februari
nane na tisa likimshutumu Rais Kikwete kwamba ameshindwa kutimiza wajibu
wake wa kuwalinda tembo na faru,” alisema Dk. Mfutakamba.
Miongoni mwa
tuhuma zilizotolewa na gazeti la Daily Mail ambazo Mchungaji Msigwa
anataka zijibiwe kwa vielelezo badala ya kauli ni juu ya watu walio
karibu na Rais Kikwete wanaohusika katika biashara haramu ya meno ya
tembo, lakini hawachukuliwi hatua.
Tuhuma
nyingine ni kuwa ndege iliyomleta Rais wa China mwaka jana iliondoka na
shehena ya pembe za ndovu ambayo ilipakiwa na maofisa waliokuwa kwenye
ndege hiyo.
Tuhuma
nyingine za gazeti hilo ambalo lilimnukuu Msigwa ni kwamba CCM na
serikali yake ni wanufaika wa mradi wa ujangili kwa lengo la kutafuta
fedha ya uchaguzi ujao na kwamba ujangili umeongezeka zaidi katika
kipindi cha utawala wa Rais Kikwete.
JK atoa kauli nzito
Katika hatua
nyingine, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa hataruhusu shehena za pembe
za ndovu zilizokamatwa katika matukio mbalimbali ya kupambana na
ujangili, kuuzwa kwani bora shehena hiyo ichomwe moto.
Pia alisema
anakwenda nchini London, Uingereza kuwaomba wasaidie kuvunja mtandao wa
masoko makubwa ya biashara ya meno ya tembo na faru yaliyoshamiri
katika nchi za mataifa makubwa.
Rais Kikwete
alisema hayo juzi usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere akiwa safarini kuelekea nchini London, Uingereza kwa
ajili ya kufanya mazungumzo ya kukomesha biashara ya meno ya tembo na
faru na mauaji yake.
Rais pia
alitaja masoko makubwa ya meno ya tembo kuwa ni pamoja na Thailand,
Vietnam na China na kuongeza kwamba endapo masoko hayo yatafungwa, basi
Tanzania na nchi nyingine mauaji ya wanyama hao hayatakuwepo.
Akizungumzia
kuhusu kutoruhusu uuzaji wa shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa
kwenye operesheni mbalimbali nchini, Rais Kikwete alisema hataruhusu
kuyauza na kama hayatakuwa na kazi nyingine ya kufanya ni bora yachomwe
moto.
“Kamwe
sitatoa kibali cha kuuza pembe za ndovu na faru ili kusaidia kudhibiti
ujangili ambao chanzo chake kikubwa ni kuwepo kwa soko kubwa la bidhaa
hiyo duniani,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo
alisema kuwa katika kipindi cha miaka ya nyuma Tanzania ilipiga hatua ya
kupambana na ujangili lakini mafanikio hayo yaliharibiwa baada
ya kurudi tena kwa biashara ya meno ya tembo katika mataifa makubwa ya nje.
ya kurudi tena kwa biashara ya meno ya tembo katika mataifa makubwa ya nje.
Alisema
katika kipindi cha miaka ya 1970 hadi 1980 mara baada ya nchi kupata
uhuru mwaka 1961, kulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini waliuawa
wote na kubakia 50,000.
Aliendelea
kueleza kuwa katika kipindi cha mwaka 1989, serikali iliingiza jeshi
katika Operesheni Uhai na kuweka mikakati mbalimbali ya kupambana na
ujangili ndipo mafanikio yalianza kuonekana.
Akizungumzia
kwa upande wa faru, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi
ya Serengeti ambao walikuwa jike, na baadaye aliingia faru dume kutoka
Ruaha, kuanza kuzaliana hadi wakafikia 32 na kuweka historia.
Rais Kikwete
pia alizindua mabango yanayohamasisha kuacha mauaji ya tembo na faru
yatakayoenezwa sehemu mbalimbali ya nchini ambayo yapo chini ya
usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Awali
akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa mabango hayo, Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo la mabango hayo
ni kutaka kuwahamasisha wananchi kushiriki katika harakati za kupambana
na ujangili.
0 comments:
Post a Comment