Thursday, 13 February 2014

MAJINA 40 YA VIJANA WATAKAOSHIRIKI SHINDANO LA MAISHA PLUS

Filled under:



MAJINA 40 ya vijana watakaoshiriki shindano la Maisha Plus 2014, pamoja na 30 ya washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula yametangazwa rasmi kabla ya baadaye kufanyiwa mchujo.

Akitangaza majina hayo jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya DMB, Masoud Ally  ‘Masoud Kipanya’, alisema mchakato wa kuwapata washiriki hao mwaka huu ulikuwa mkali na wenye ushindani kutokana na kupokea maombi mengi ya vijana, ambao wengi wao walijaza fomu katika vituo na kupitia mitandao karibu nchi nzima.

“Katika maombi hayo, jumla ya majaji 25 waliweza kuchuja na kisha kupata majina 40. Kwa mara ya kwanza tumepokea maombi mengi karibu nchi nzima. Jopo hilo lilifanya hivyo hivyo na kwa washiriki wa Mama Shujaa wa Chakula, ambapo wao walipatikana washiriki 30,” alisema Masoud Kipanya.

Kipanya alifafanua kuwa mwaka huu hatua ya awali ya shindano hilo kutakuwa na makundi mawili, ambayo kila moja litakuwa na vijana 20, ambako watapigiana kura wao wenyewe kwenye vijiji maalumu watakapopelekwa ili kubakia washiriki tisa kwa kila kundi.
“Tutakuwa na washiriki 20, wataishi kwenye Kijiji maalumu huko Visiwani Zanzibar na pia  kutakuwa na kijiji kingine huko mkoani Iringa ambapo vijana 20 wengine watakaa huko,” alisema Masoud.
Aliwataja washiriki hao na mikoa wanayotoka kwenye mabano kuwa ni Zaharani Yusuph (Tanga), Yassin Suddi (Dar es Salaam), Thomas Mgazwa (Dodoma), Shishira Mnzava (Morogoro), Shida Mganga (Dodoma), Shaaban Masoud Shaaban (Zanzibar), Seif  Salum (Tabora), Scholastica Deusidedith (Geita), Salum Johari (Mtwara) na Said Salum (Katavi).

Wengine ni Otilia Simime, Osama Norman (Mbeya), Ngoma Abdallah (Kigoma), Nelson Daniel (Dar es Salaam), Moureene Daud (Kagera), Mohamed Lipembe (Lindi), Mbonimpanye Nkoronko (Rukwa), Mary Kavishe (Manyara), Mariam Moses (Shinyanga), Joyce Mushi (Arusha), John Malima (Geita), na Jane Julio Kalinga (Iringa).

Kipanya aliwataja wengine kuwa ni Hyasinta Hokororo (Mtwara), Frederick Ndahani (Singida), Flora John (Singida), Fadhil Isanga (Kilimanjaro), Farid Ally (Pwani), Rahmn Kaite Mwadini (Zanzibar), Elizabeth Joachim (Tabora), Ellymathew Kika (Njombe),  Douglas Msalu (Arusha), Charles Daniel (Simiyu), Boniphace Nyankena (Dar es Salaam), Bakari Khalid (Shinyanga), Ausi Noyo (Ruvuma), Asumta Mwingira (Dar es Salaam), Anastazia John (Mara), Ally Thabit (Mwanza), na Adolph Anacleth (Mwanza).

Aliongeza kuwa baada ya mchujo na washiriki kubaki 18, baadaye wataongezwa washiriki wengine  12, kutoka nchi nne za Afrika Mashariki zikiwemo Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda, ambao watakaa kwa zaidi ya miezi miwili huku mshindi kwa mwaka huu akitarajiwa kuondoka na kitita cha  sh milioni 20.

0 comments:

Post a Comment