Wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram
kaskazini mashariki mwa Nigeria wametuhumiwa kushambulia shule moja na
kuwaua wanafunzi kadhaa.
Polisi nchini Nigeria wameliambia Shirika la
Habari la Uingereza, Reuters kwamba wote waliouawa ni wavulana na kwamba
baadhi ya miili ya wanafunzi hao imeungua na kubaki majivu.
Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema shambulio hilo limefanyika katika jimbo la Yobe.
Wakaazi wa mji wa Buni Yadi katika jimbo hilo, wamesema washambuliaji hao walivamia usiku na kuwachinja baadhi ya wanafunzi.
Wamesema baadhi waliuawa kwa kupigwa risasi.
Walimu katika chuo cha serikali ya shirikisho
katika mji wa Buni Yadi wameliambia shirika la habari la AP kwamba
wanafunzi wapatao 40 waliuawa katika shambulio hilo ambalo lilianza
mapema Jumanne asubuhi.
Jeshi limethibitisha kwamba shambulio hilo
limetokea katika hosteli za wanafunzi lakini limesema haliwezi kutoa
taarifa zaidi kwa sasa.
Kundi la Boko Haram limekuwa likishutumiwa
kuendesha vitendo vya mauaji kaskazini mwa Nigeria, yakiwemo mauaji ya
mapema mwezi huu katika jimbo la Yobe.
Boko Haram, lina maana ya"Elimu ya Magharibi ni
dhambi" katika lugha ya Kihausa, mara kwa mara limekuwa likishambulia
shule katika siku za nyuma.
Watu kadhaa wameuawa katika mashambulio mawili
yaliyotokea wiki iliyopita. Katika tukio moja, wanamgambo hao wa Boko
Haram, waliteketeza kijiji kizima na kuwapiga risasi wakaazi wa eneo
hilo waliokuwa wakijaribu kutoroka.
0 comments:
Post a Comment