Raia wa Ugiriki, Alexandria Athanasios (30), amekamatwa kwa tuhuma za
kukutwa na kilo 5.3 za dawa za kulevya aina ya heroine katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Meneja Usalama wa uwanja huo, Clemence Jingu, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kwamba raia huyo wa kigeni alikamatwa juzi saa 3:00 usiku
uwanjani hapo.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa,
akifafanua zaidi tukio hilo alisema Athanasios alikamatwa wakati
akijiandaa kusafiri na ndege ya shirika la Swiss Air kutoka Dar es
Salaam kwenda Ugiriki kupitia Zurich.
Alisema mtu huyo alikamatwa na maofisa wa uwanja huo kwa kushirikiana na polisi wakati akikaguliwa mizigo yake.
Kamanda Nzowa alisema mtu huyo anaendelea kushikiliwa na polisi na
kwamba uchunguzi wa kujua dawa hizo zina thamani gani unaendelea
kufanyika na upepelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kukamatwa kwa dawa hizo kumekuja wiki tatu ndani ya mwezi huu tangu raia
12 wa Pakistan na Iran walipokamatwa na shehena ya dawa za kulevya
zaidi ya kilo 201 katikati ya Dar es Salaam na Zanzibar katika Bahari ya
Hindi.
Kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha dawa kulizua taharuku kubwa katika
Jiji la Dar es Salaam na kusababisha wananchi kulazimika kukimbilia
katika Bandari ya Dar es Salaam kushuhudia tukio hilo.
Watu hao walikamatwa wakiwa katika jahazi ijulikanayo Aldanial iliyotokea nchini Iran mali ya Raisee, raia wa Iran.
Waliokamatwa katika tukio hilo ni Muhamad Hassan (30), Abdul Nabii (30),
Fahir Muhamad (34) na Rahim Baksh (30), wote raia wa Pakistan.
Raia wa Iran waliokamatwa ni Abdulsamed Badreuse (47), Ayoub Hot (50),
nahodha wa jahazi hilo, Hazra Azat (60), Nahim Mussa (35), Khalid Ally
(35), Kher Muhamad (75), Said Muhamad (34) na Murad Gwaharam (38).
Tuesday, 25 February 2014
RAIA WA UGIRIKI ATUHUMIWA BAADA YA KUKUTWA NA UNGA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment