Utafiti umebaini kuwa matumizi ya dawa za kulainisha nywele 'relaxer’
ni chanzo cha wanawake kuota uvimbe kwenye kizazi unaojulikana
kitaalamu kama ‘fibroids’.
Kadhalika kuweka dawa hizo kwenye nywele kunasababisha mabinti kuvunja ungo wakiwa na umri mdogo.
Utafiti huo ulifanywa hivi karibuni na kuchapishwa na Jarida la Marekani la Magonjwa ya Binadamu.
Jarida hilo la Annals of Epidemiology-Journal, limeandika kuwa
wanasayansi waliwachunguza wanawake Wamarekani weusi kuanzia mwaka 1997
hadi 2009 na kubaini kuwa kuna viwango vya zaidi ya mara tatu vya kuota
uvimbe wa kizazi kwa wanawake weusi kunakotokana na dawa za ‘relaxer’
ikilinganishwa na wanawake wengine.
Walibaini kuwa uvimbe huo unahusishwa na matumizi ya kemikali za
nywele za ‘relaxer’ na viambata vyake ambavyo huingia mwilini kupitia
ngozi ya kichwa iliyojeruhiwa kwa michubuko na kuunguzwa na dawa.
Jarida liliripoti kuwa Waamerika weusi wanapata hedhi kabla ya
kufikia miaka 10 pia walibainika kukumbwa na ‘fibroids’ na kuanza kupata
siku zao za mwezi wakiwa wadogo kuliko ilivyotakiwa kutokana na dawa
hizo.
Wanawake 300 wakiwamo Wamarekani weusi na weupe, wengine wa asili
ya Caribbean na Hispania waishio jijini New York walichunguzwa katika
utafiti huo.
Matokeo yalibainisha kuwa licha ya wanawake kupata hedhi wakiwa na
umri kati ya miaka nane hadi 19 lakini kwa upande wa Waamerika weusi
wamegundulika kuwa wanawahi kupata hedhi kuliko watu wa rangi nyeupe
kutokana na kutumia ‘relaxer’ na viambata vyake.
Viambata hivi ni kama mafuta ya nywele, dawa za 'steaming', ‘spray’ losheni na ‘conditioner.’
Kinachoonekana katika utafiti huo ni uhusiano baina ya ‘relaxer’ na
kuwepo uvimbe wa aina za ‘fibroid’ na `tumour’ na mabinti kupevuka
mapema lakini hakuna maelezo ya usababishaji wa magonjwa na hali hiyo.
Kufuatia maelezo hayo wataalamu wanakosoa kuwa sekta ya urembo na
vipodozi vya nywele haidhibitiwi na Mamlaka ya Marekani ya Udhibiti wa
Chakula na Dawa (FDA).
Wanaeleza kuwa hakuna utaratibu maalumu wa kufuatilia na kufahamu
jinsi kemikali za kutengeneza dawa na vipodozi vya nywele za watu weusi
zilivyo na madhara yake.
FIBROID
Unaoota ndani ya kizazi, mara nyingi hauna seli za saratani na
wataalamu wamegundua kuwa unaota kutokana na nyuzi za misuli ya mwili.
Fibroid zina sura ya mapafu ya mnyama ni nyama laini zinapoota
huanza na ukubwa wa njegere lakini hukua na kuongezeka hadi kimo cha
tikitimaji.
Katika taarifa hiyo ya relaxer iliyoko kwenye mtandao, baadhi ya
walioijadili walipendekeza kufanyike utafiti zaidi wa madhara yake kwa
watumiaji. Walisema nywele za asili ni bora na zinalinda afya na uzuri
wa mtu bila kutumia dawa.
Muuguzi Deborah Jones wa Virginia, Marekani, anasema madaktari
wengi wamewaasa watu kuachana na matumizi ya kemikali kama relaxer ili
kuepuka uwezekano wa kupata maradhi ya saratani.
“Wengi wanadhani kuwa nywele za kipilipili ni vigumu kuzitunza na
zinapoteza muda kuzishughulikia , lakini kama utatumia zaidi ya saa
mbili saluni ili kuwekewa relaxer, kukausha , kusetiwa kama ungekuwa na
kipipili usingepoteza muda mwingi kiasi hicho.”
Ni bora kama madaktari watawahimiza watu kuachana na kemikali hizi
za relaxer na dawa za kubadilisha rangi ambazo lengo lake ni kulazimisha
watu kutumia fedha nyingi kwenye vipodozi badala ya mambo muhimu ya
maisha.
WATANZANIA
Kwa Watanzania ni wakati wa wanawake kujihoji hasa wale
wanaotumia relaxer muda wote, wakiwa wajawazito, wakinyonyesha na pia
huwapaka mabinti zao.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Wakala wa Mkemia Mkuu wa
Serikali wachunguze vipodozi vya nywele ambavyo kama ilivyo kwa
Marekani yapo maelezo kuwa havidhibitiwi na mamlaka ya dawa ya FDA.
0 comments:
Post a Comment