Viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri,
wameingia kwenye kashfa inayowaweka katika wakati mgumu, baada ya
kubadili matumizi ya nyumba za Serikali walizonunua, kinyume na mikataba
inavyoeleza.
Nyumba hizo ambazo zilianza kuuzwa mwaka 2002 enzi
ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ziliuzwa kwa
mawaziri, makatibu wakuu na watumishi wengine wa ngazi mbalimbali za
umma.
Mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za
Serikali inaeleza kuwa, mfanyakazi wa Serikali anaponunua au kukopeshwa
nyumba, hatakiwi kubadili matumizi au kuuza hadi baada ya miaka 25
kupita.
Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na 9 na
10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba
hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na mitano (25), kuanzia
tarehe ya hatimiliki.
Alitafutwa Waziri wa Ujenzi, John
Magufuli mwenye dhamana na nyumba za Serikali kwa muda wa miezi miwili
kutoa ufafanuzi wa suala hilo bila mafanikio, huku akitoa sababu
mbalimbali kwa mwandishi kukwepa kuzungumzia suala hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson
Lwenge alisema kuwa anahitaji kupata ripoti kamili kutoka kwa Wakala wa
Nyumba za Serikali (TBA), ili ajionee mikataba na afahamu ni wapi
ilipovunjwa.
“Serikali ina nia nzuri kabisa kuwauzia watumishi
wake nyumba, lakini kama kuna mikataba inakiukwa, basi TBA inafahamu kwa
kina ni kwa vipi watu hao wachukuliwe hatua,” alisema.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, viongozi
wengi ambao nyumba zao zipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na
Mwanza wamezibadili matumizi na kuwa za biashara.
Kwa Jiji la Dar es Salaam baadhi ya nyumba
zilizouzwa kwa vigogo hao wa Serikali na kubadilishwa matumizi zipo
katika maeneo ya Oysterbay.
Mwandishi alishuhudia baadhi ya nyumba hizo
zikiwa zimebadilishwa matumizi na kuwa klabu za starehe, kupangishwa
taasisi au balozi, huku nyingine zikiwa tayari zimeuzwa.
Moja ya nyumba hizo ni ya aliyewahi kuwa Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohamed Seif Khatib,
iliyopo Oysterbay, Mtaa wa Bongoyo katika Barabara ya Hillpark. Nyumba
hiyo kwa sasa imevunjwa na kujengwa klabu na baa iitwayo Ocasa.
Alipoulizwa kuhusu nyumba hiyo na mkataba wake
unavyosema, Khatib alisema kwamba hajavunja sheria yoyote kwa sababu
hajauza
Alifafanua kuwa yeye amebadili matumizi sehemu ndogo ya nyumba
hiyo huku akimtaka mwandishi aandike tu kuhusu sehemu kubwa na siyo
mabadiliko aliyodai ni madogo.
“Nyie waandishi ndivyo mlivyo, kwa nini msiandike
mazuri yetu. Mnapenda kuandika mambo mabaya tu, mnataka tuishi
kimaskini. Nyumba imejengwa tangu enzi za ukoloni, mnataka mpaka leo
ibaki hivyohivyo?” alihoji.
Eneo la Kinondoni, palipokuwa na nyumba ya
aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya katika Serikali ya Rais Kikwete,
nayo kwa sasa imevunjwa na kujengwa ghorofa, huku kibao cha mkandarasi
kikionyesha kuwa ujenzi wa jengo la biashara unaendelea.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha
kuwa nyumba nyingine za viongozi wa Serikali zilizobadilishwa matumizi
zipo eneo la Msasani na Masaki.
Nyumba nyingine iliyobadilishwa matumizi
inamilikiwa na waziri mmoja eneo la Barabara ya Hindu, Kinondoni mkabala
na Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ambayo imebadilishwa na kujengwa
nyumba za kupangisha watu.
Mjini Arusha baadhi ya nyumba za Serikali zilizouzwa na kubadilishwa matumizi zipo eneo la Uzunguni.
Moja ya nyumba hizo ipo karibu na Ikulu ndogo
mjini humo, ambayo hivi sasa imebadilishwa na kuwa baa. Nyumba hiyo ipo
Mtaa wa Haile Selassie.
Katika Jiji la Mwanza, nyumba zilizobadilishwa matumizi zipo katika eneo la Isamilo na Kapiripointi.
0 comments:
Post a Comment