Monday, 27 January 2014

POLYCARP KARDINALI PENGO NI MGONJWA

Filled under:

Polycaro Kardinal Pengo
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (70) ni mgonjwa, imetangazwa.

Taarifa ya kuugua kwa Kardinali Pengo, kiongozi wa kiroho anayeaminika kwa kukosoa uovu unaofanywa kwenye jamii, imetangazwa na Askofu Msaidizi wa kanisa hilo jimboni humo, Mhashamu Titus Mdoe.

Mdoe, alitoa taarifa hiyo wakati wa misa takatifu iliyofanyika jana kwenye kigango cha Nzasa, parokia ya Temboni jimboni humo.

Misa hiyo ilikuwa mahususi kwa ajili ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi na huduma za kiroho kwa kigango hicho kinachotarajiwa kupandishwa hadi ili kiwe parokia.

Mhashamu Mdoe hakutaja ugonjwa unamsumbua Kardinali Pengo, lakini aliwataka Wakatoliki na watu wenye mapenzi mema, kuendelea kumuombea ili apate nafuu.

Alisema ugonjwa wa Kardinali Pengo unaweza kuchangiwa pia na hali ya kuelekea katika uzee, ingawa sababu hiyo haijafikia kuwa chanzo kikuu cha kumfanya augue.
Katika hatua nyingine, Askofu Mdoe alisema utumishi wa umma ulio bora unapaswa kuelekezwa katika kutatua umasikini na kero zinazoikabili jamii, hivyo kufikia tarajio la kuwa maisha bora.

Pia alikosoa tabia ya baadhi ya viongozi hususani watawala, kupiga picha zenye mwelekeo wa kushiriki na kutatua kero za jamii, huku lengo likiwa ni kupata nafasi kwenye vyombo vya habari.

Alisema miaka 52 ya Uhuru ilitosha kwa kutatua umasikini na kero nyingine zinazoikabili nchi.

Badala yake, alisema walio katika dhamana ya kufanikisha azma hiyo, wameshindwa kufikisha tumaini la maendeleo kwa wananchi hasa wa vijijini, licha ya ukweli kwamba maendeleo mijini yanakua kwa kasi.

Mhashamu Mdoe, alisema watu kama maafisa kilimo ambao damu zao zipo kwa kuwatumikia watu, hawapaswi kukaa maofisini wakiwa wamevaa suti, bali kuhakikisha wantekeleza wajibu wa kuwahudumia wakulima.

Alisema kuna maeneo mengi ya nchi yasiyofikiwa na mahitaji muhimu kwa jamii kama umeme, maji, afya na elimu bora, hivyo kuwafanya wasinufaike na matunda yanayotokana na Uhuru na rasilimali za nchi.

0 comments:

Post a Comment