MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amekionya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na serikali yake kuacha hila zozote zile ambazo zitasababisha kuvunjika
kwa mchakato wa katiba mpya unaoelekea hatua ya Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema waache kufikiria kufanya hivyo
kwani kwa hatua iliyofikia, Watanzania hawako tayari kurudi nyuma
kuendelea na katiba ya sasa.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA taifa
aliyasema hayo juzi jioni wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya
ya Ngara, mkoani Kagera, ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya Movement For
Change (M4C) iliyopewa jina la Pamoja Daima, ambayo inaendeshwa na
viongozi wa chama hicho nchi nzima, wakigawanyika katika timu sita –
tatu zikitumia usafiri wa helkopta na nyingine zikiwa ardhini.
Mbowe alisema kuwa yupo tayari kuwa wa
kwanza kufungwa kwa kosa la kudai katiba mpya iwapo serikali itaweka
mazingira ya hila ambayo yatalazimisha kukwamisha mchakato wa kupata
katiba mpya, hivyo Watanzania kulazimika kuendelea na katiba ya zamani
ya mwaka 1977.
Alisema kuwa watawala wasitumie hila na
mwanya wowote kuitia nchi majaribuni kwa kulazimisha watu ‘kuishi’ na
katiba ya sasa aliyosema imekosa uhalali wa kisiasa na kisheria, bali
wanatakiwa kuhakikisha mazingira mazuri yanapatiana kwa Watanzania
kujiamulia wanavyotaka kuongozwa, huku akisisitiza kuwa katiba ni uhai
wa taifa, si matakwa ya chama chochote cha siasa wala mtu binafsi.
Mbowe alisema kuwa Watanzania wengi
wamependekeza kuwapo kwa shirikisho la serikali tatu katika rasimu ya
katiba mpya, lakini akadai kuwa zipo njama zinazofanywa za kuchakachua
maamuzi hayo ya wananchi kwa ajili ya kuilinda CCM.
Alisema iwapo hila hizo za kupindua
maoni ya wananchi zitafanikiwa kupenyezwa kupitia bungeni, yuko tayari
kuungana na Mtanzania yeyote kuzunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi
waikatae rasimu hiyo.
Alisisitiza kwa kusema kuwa endapo
wananchi wataikataa katiba hiyo, pia hawatakuwa tayari kurudi kuendelea
kutumia katiba ya zamani inayotumika hivi sasa kama ambavyo serikali
imekwishasema.
“Watawala lazima wajue. Watanzania hawa
ambao wameipigania na kuililia katiba mpya kwa muda mrefu sasa, hawako
tayari tena kurudi nyuma. Maana kuna kipengele cha sheria kimewekwa
kwamba mchakato huu wa sasa ukishindikana kwa maana kwamba wananchi
wakipiga kura ya maoni kuikataa rasimu itakayokuwa imepitishwa bungeni,
eti tunaendelea na katiba ya zamani.
“Kwa hiyo kwa kutumia mwanya huo, kuna
watu, tena wanaongozwa na chama kilichoko madarakani, wamejipanga
kuhakikisha kwamba wanachakachua maoni ya wananchi yaliyotolewa ili
ikifika wakati wa kura ya maoni wananchi waikatae, na hivyo mchakato
wote unafeli, tunarudi kwenye katiba ya zamani na hivyo kuanza mwanzo
tena mchakato wote.
“Kwa kweli Ngara ninawaambia kwa hilo
hatuko tayari. Wananchi wametoa maoni yao mengi mengi kuhusu siasa,
uchumi na jamii yazingatiwe kwenye katiba mpya, lakini watawala wako
tayari kuingiza nchi majaribuni kwa sababu tu wanataka kuendelea kulinda
ulaji wao. Wanataka uhai wa chama chao. Hatutakubali.
“Tena wanaojipanga kuchakachua ni wale
wanaokataa serikali tatu, eti sio sera ya chama chao, alaah! Wanapata
wapi jeuri hii ya kutaka katiba ya nchi iongozwe na sera za vyama vya
siasa na kwa nini chama chao ndiyo kielekeze katiba iweje badala ya
wenye katiba ambao ni wananchi wenyewe?
“Niko tayari. Nitakuwa wa kwanza
kufungwa endapo katiba inayoandaliwa sasa itachakachuliwa na baadhi ya
watu kwa sababu tu hawataki serikali tatu, kwani nitazunguka nchi nzima
kuhamasisha wananchi kuikataa na baada ya kuikataa pia hatutakuwa tayari
kurudia ile ya zamani.
“Haiwezekani Watanzania walio wengi
wakatoa maoni kuhusu siasa za nchi, kuhusu uchumi wa nchi na mambo ya
kijamii ili watengeneze mazingira ya fursa za maendeleo kwa katiba
wanayoitaka wao, halafu wengine, kikundi kidogo kwa maslahi ya chama
chao waichakachue eti tu kwa sababu ya maslahi yao binafsi ya kutaka
kujitengenezea mazingira ya ulaji.
“Katiba ni uhai wa taifa hili. Ni uhai
wa Watanzania wote siyo ya chama chochote cha siasa au ya mtu fulani,
mbona Zanzibar wenyewe wametengeneza katiba yao kwanini na sisi
tusingeneze ya Tanganyika? Walikuwa wapi wakati masuala yote
yanayotishia kabisa Muungano yanazidi kukomaa?” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa haiwezekani kutumia muda
mwingi na gharama kubwa ya fedha kuandaa katiba hiyo halafu watu
wengine wakaichakachua, na kwamba hata kama katiba hiyo itakataliwa,
haiwezekani kuendelea kutumika ile ya zamani inayotumika sasa, bali ni
lazima itaipasa serikali kuangalia utaratibu mwingine wa kuhakikisha
katiba mpya inapatikana.
“Wazo la kurudi katika katiba ya zamani
halipo kabisa, kama Serikali ya CCM inajidanganya kwamba watachakachua
katiba inayoandaliwa sasa halafu tukarudi kutumia ile ya zamani, hiyo
haipo na itawagharimu,” alisisitiza.
Kadhalika Mbowe alisema kuwa watazunguka
nchi nzima kuwahamasisha Watanzania kususia zoezi la upigaji kura ya
maoni ya katiba endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itashindwa
kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.
Alisema kupiga kura ni haki ya msingi ya
Watanzania, na kwamba hadi sasa zaidi ya Watanzania milioni tano na
laki tatu hawana uwezo wa kupiga kura kwa sababu hawana shahada ya
kupigia kura.
0 comments:
Post a Comment