Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Dk. Amani alisema ameshangaa vyombo vya habari kutangaza kuwa amejiuzulu umeya ilhali yeye bado ni Meya halali wa Manispaa ya Bukoba.
Wiki iliyopita vyombo vya habari nchini vilitangaza kuwa Dk Amani amejiuzulu nafasi yake ya umeya baada ya Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kumhusisha na mikataba yenye utata.
“Nimeshangaa vyombo vya habari vimezusha na kuandika eti Meya Bukoba ang’oka,” alisema na kuongeza kuwa habari hizo hazikuwa na ukweli wowote.
Alisema hang’ang’anii umeya lakini anatetea haki yake na kwamba hataki kuonewa.
Dk Amani alisema kuwa ripoti ya CAG inayomhusisha yeye na mikataba ya kifisadi haina ukweli na kwamba ina lengo la kumchafua.
Alisema kuwa baadhi ya madiwani katika manispaa ya Bukoba wamekuwa wakitumika ili kumng’oa yeye katika kile alichokieleza kuwa ni uoga wa baadhi ya viongozi wa CCM kuwa anaweza kugombea ubunge katika Jimbo la Bukoba Mjini.
Dk Amani alisema anashangaa kuwa wakati yeye analalamikiwa na viongozi wa chama na ripoti ya CAG kuna baadhi ya madiwani ambao wamekosa sifa za kuwa madiwani lakini hawafukuzwi.
Alisema kuwa kuna baadhi ya madiwani ambao hawajahudhuria zaidi ya vikao vitano, hali ambayo inawafanya wakose sifa za kuwa madiwani lakini cha kushangaza pamoja na yeye kulalamika kuhusu madiwani hao katika ngazi za juu bado hawaondolewi katika nafasi zao.
0 comments:
Post a Comment