Wednesday, 22 January 2014

MAJINA YA WAJUMBE WA KATIBA WALIOTEULIWA NA JK YAPO NJIANI,2500 WACHUJWA

Filled under:



Majina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete sasa yatawekwa hadharani wiki ijayo.

Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete atakuwa na mtihani mgumu wa kuteua majina ya wajumbe hao kutoka asasi mbalimbali kutokana na idadi kubwa ya majina yaliyowasilishwa Ikulu na asasi hizo kulingana na nafasi ndogo za kuteua.

Jumapili iliyopita, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa majina ya watu 2,722 yaliyowasilishwa kwa Rais kutoka makundi hayo yalikuwa yanaendelea kuchambuliwa.

Hiyo ina maana Rais Kikwete ana kazi ngumu ya kuchuja majina ya watu 2,521 ili kupata idadi ya kisheria ya wajumbe 201 (asilimia 7.4) watakaoingia katika Bunge Maalumu la Katiba.

Hatua hiyo inatarajiwa kuchukuliwa baada ya Rais Kikwete kukamilisha uteuzi wa wajumbe hao na pia baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, hatua hiyo inatarajiwa kuchukuliwa kwa kuzingatia kifungu cha 22 (3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Toleo la 2013.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anakusudia kukamilisha uteuzi wa wajumbe hao baada ya kushauriana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mwanzoni mwa wiki ijayo na majina hayo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama kifungu cha 22 (3) cha sheria iliyotajwa inavyomtaka kufanya,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilinukuu kifungu cha 20 (2) cha sheria hiyo na kusema kinamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha kwenye Gazeti la Serikali rasimu ya katiba ndani ya siku 30 baada ya kukabidhiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Taarifa iliyotolewa leo (jana) na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, inaeleza kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, alikabidhiwa rasimu ya katiba tarehe 30 Desemba, 2013, na ataichapisha kwenye Gazeti la Serikali litakalotolewa Ijumaa (kesho), tarehe 24 Januari 2014,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilinukuu kifungu cha 22 (1) (c) cha sheria hiyo na kusema kinampa madaraka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar kuteua wajumbe 201 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka miongoni mwa majina yanayopendekezwa kwao na makundi yaliyotajwa ndani ya sheria hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa Jumapili iliyopita mgawanyo wa nafasi za wajumbe ni kama ifuatavyo: Asasi zisizokuwa za kiserikali zinatakiwa kutoa wajumbe 20, majina yaliyowasilishwa ni 1,185; taasisi za kidini wajumbe 20 majina yaliyowasilishwa ni 277; vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu wajumbe 42 majina yaliyowasilishwa ni 126.

Makundi mengine na majina yaliyowasilishwa kwenye mabano ni taasisi za elimu wajumbe 20 (82); makundi ya watu wenye ulemavu wajumbe 20 (70); vyama vya wafanyakazi wajumbe 19 (69); vyama vinavyowakilisha wafugaji wajumbe 10 (43); vyama vinavyowakilisha wavuvi wajumbe 10 (45); vyama vya wakulima 20 (115) na makundi yenye malengo yanayofanana wajumbe 20 (710).

Kundi la kuteuliwa na Rais lina wajumbe 201, wakati sheria ya mabadiliko ya katiba inataka Bunge Maalumu la Katiba kuwa na jumla ya wajumbe 635.

Makundi mengine ni wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye wabunge 358 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lenye wajumbe 76.

Aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alisema kuwa kati ya wajumbe 201 kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, nusu watakuwa wanawake na nusu nyingine watakuwa wanaume.

Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70, linatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao kwa ajili ya kujadili na kuipitisha rasimu ya pili ya katiba iliyopendekezwa. Sheria hiyo inamtaka Rais akishakabidhiwa rasimu ya katiba ndani ya siku 31 achapishe katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, ndani ya siku 21 Rais ataitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa.

Baada ya rasimu ya pili kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, itaitishwa kura ya maoni, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa. 

0 comments:

Post a Comment