Uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Sombetini umeanza kwa vurugu baada
ya wanachama watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kujeruhiwa na kundi la vijana walinzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Green
Guard.
Aidha, mgombea wa CCM kwenye kata hiyo, David Lesikari, akiwa na watu
wengine anadaiwa kuwashambulia na kitu chenye ncha kali wanachama
wawili wa CHADEMA na kumjeruhi mwingine kichwani na mgongoni.
Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Arusha, Ephata Nanyaro, aliwaeleza
waandishi wa habari jana kuwa vurugu hizo zilitokea Januari 20 mwaka huu
na kwamba licha ya wanachama wao kuumizwa, Jeshi la Polisi liliwakamata
na kuwageuzia kesi kuwa wao ndio waliofanya vurugu.
Alisema siku hiyo saa nane mchana mwanachama wao, Vitalis Bernad,
alipigwa shoka la kichwa na kijana aliyedai kuwa kiongozi wa CCM wakati
akipita kwenye kona ya Mbauda akiwa kwenye pikipiki yenye bendera ya
CHADEMA wakielekea kwenye mkutano wa mgombea wa chama chao, Ally
Bananga.
“Kwa bahati Bernard alikuwa amevaa kofia ngumu za waendesha pikipiki
hivyo hakuumia sana lakini watu waliokuwa pale walijaribu kumkimbiza
mhusika lakini hawakufanikiwa, kwani alikimbilia kwenye ofisi ya CCM
ambapo walitokea kundi la watu wenye mapanga kutoka ndani ya ofisi hizo
jambo lililowafanya wananchi kutawanyika kwa hofu,” alisema Nanyaro
Alisema Bernard akiwa na viongozi wa CHADEMA walienda polisi kufungua
taarifa namba Ar/RB/982/2014 kwenye kituo kidogo cha Mbauda karibu na
ofisi hizo za CCM ambapo waliwaeleza polisi kuwa mtuhumiwa yuko ndani ya
ofisi hizo lakini hawakutaka kwenda kumkamata.
Mwenyekiti huyo wa wilaya alisema siku hiyo hiyo saa 12 jioni
Wanachadema wawili, Loserian Laisi na Mozec Joseph wakitokea kwenye
mkutano wa kampeni wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki walivamiwa na
kundi la watu wakiongozwa na mgombea wa CCM ambapo waliwashambulia kwa
mapanga na silaha za jadi.
Nanyaro alisema katika tukio hilo Loserian alikatwa kichwani na
kiunoni kwa kitu chenye ncha kisha kutelekezwa migombani kabla ya
kusaidiwa na wasamaria wema waliompeleka Kituo cha Polisi cha Sombetini
kupata fomu ya matibabu (PF3) na kwenda hospitali.
“Polisi bila weledi walichukua maelezo kwa saa mbili huku Loserian
akiwa kwenye maumivu na damu zikimtoka hata hivyo alipatiwa matibabu
katika hospitali ya Kaloleni, akiwa anaendelea na matibabu polisi
walifika hospitalini na kumchukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi na kumweka
rumande,” alilalamika Mwenyekiti huyo wa CHADEMA.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas,
alikiri ofisi yake kupokea taarifa za vurugu za jioni huku akibainisha
kwamba taarifa za tukio la mchana hakuzipata.
Akizungumza na mwandishi, Kamanda Sabas alisema kwenye tukio
hilo la jioni vijana wa CHADEMA wakiwa kwenye pikipiki mmoja alishuka na
kumpiga vibao mgombea wa CCM, Lesikari, ambapo wananchi walioona
walipandwa na hasira hivyo kuwashambulia na kukiri kwamba vijana wa
CHADEMA kuhojiwa na polisi kuhusu tukio hilo.
“Unaweza kupigwa karibu ya kituo cha polisi haimaanishi waliokupiga
ni polisi, hivyo huyo inawezekana kabisa alipigwa hapo kona ya Mbauda
karibu na ofisi za CCM lakini wahusika si Wana CCM, kwenye kesi
kinachotafutwa ni ushahidi si hisia,” alisema kamanda huyo.
0 comments:
Post a Comment