KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape
Nnauye, amepoteza uhalali wake wa kuendelea kushika wadhifa huo,
kutokana na utendaji wake kukinzana na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete
Hali hiyo inatokana na taswira inayozidi kujitokeza kati ya wawili
hao katika kusimamia masuala mazito yaliyoasisiwa na chama hicho.
Kwa nyakati tofauti, umejitokeza msigano ambapo wakati Nape
akizunguka kwa wananchi mikoani kunadi msimamo wa CCM kuhusu jambo
fulani, Rais Kikwete baadaye anajitokeza na kutoa mtazamo tofauti.
Hatua hii imeibua mkanganyiko kwa wananchi, na hivyo baadhi kufikia
hatua ya kushauri Nape aachie ngazi ili kuonyesha kuwa amesalitiwa
badala ya kuendelea kuonekana adui kwa wale anaosimamia wang’olewe.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Bukoba, Dk. Azavery Lwaitama,
alizungumzia hali hiyo akisema inaonyesha kuwa hakuna mawasiliano kati
ya Rais Kikwete na sekretarieti yake ya chama.
Alisema kuwa kama kungekuwa na mawasiliano ya kutosha, rais
asingewateua tena baadhi ya mawaziri waliodaiwa na chama chake kuwa
mizigo kuendelea kushika madaraka.
Mwishoni mwa mwaka jana, wakiwa katika ziara za kuimarisha chama
mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Nape mbele ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, aliwataja baadhi ya mawaziri akiwaita mizigo
kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Katika mikutano yao tofauti ya hadhara, Nape alikwenda mbali zaidi
akisema mawaziri hao lazima waitwe mbele ya Kamati Kuu ya chama
kujieleza na kuchukuliwa hatua.
Mawaziri waliotajwa ni Christopher Chiza (Kilimo na Chakula) na Naibu
wake, Adam Malima, Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na
Prof. Jumanne Mghembe (Maji)
Lakini kama hiyo haitoshi, katika kikao cha wabunge wa CCM na Rais
Kikwete mjini Dodoma mwaka jana, mawaziri Dk. Mathayo David (aliyekuwa
wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Kawambwa walidaiwa kupwaya na
kutakiwa kuondolewa ili kunusuru chama.
Pia vikao vilivyopita mwaka jana, Bunge likiongozwa na wabunge wa CCM
walimtaja Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia
pamoja na naibu wake Agrey Mwanri kama mizigo kwa kushindwa kukomesha
ufisadi kwenye halmashauri.
Katika hatua ya kushangaza, Rais Kikwete katika mabadiliko ya baraza
lake hivi karibuni, aliwarejesha mawaziri wote watuhumiwa isipokuwa Dk.
Mathayo aliyeng’oka kwa shinikizo la Bunge.
Kurejeshwa kwa mawaziri hao kumeibua mjadala mkali kwa wananchi, huku
wengi wakihoji ni kwanini rais hafanyi mawasiliano na chama chake ili
kuondoa chuki zinazoweza kujitokeza
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kusigana na CCM, kwani hata
wakati wa utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba iliyoasisiwa mwaka
2011 na kusimamiwa na sekretarieti, baadaye ilishindwa kutokana na
msimamo wa mwenyekiti huyo.
Itakumbukwa kuwa baada ya falsafa hiyo kuasisiwa, Nape na Naibu Kaibu
Mkuu wa CCM (Bara) wakati huo, John Chiligati, walizunguka mikoani
wakijiapiza kuwa watuhumiwa wa ufisadi lazima wang’oke ndani ya siku 90.
Hadi muda huo unamalizika, ni mtuhumiwa mmoja pekee, Rostam Azizi,
aliyekuwa mbunge wa Igunga ndiye aliyejiuzulu huku akiwatuhumu Nape na
Chiligati kuwa walipotosha dhana nzima.
Nape aliwataja Rostam, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kuwa ni miongoni mwa wanaotakiwa
kujivua gamba.
Pia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Pius Msekwa,
alithibitsha baadaye kuwa alikutana na Chenge, Lowassa na Rostam na
kwamba taarifa ya matokeo ya mazungumzo itawasilishwa katika vikao vikuu
vya chama.
Hata hivyo, baadaye kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC), Rais Kikwete
alisema kuwa dhana hiyo ilipotoshwa na kuonekana iliwalenga baadhi ya
watu, jambo alilosema halikuwa kweli.
Kwa msimamo huo, Lowassa, Chenge na watuhumiwa wengine walijiona
washindi na hivyo Nape na sekretarieti yake kutafsiriwa kama viongozi
waliokuwa wakiendesha siasa za chuki ndani ya chama.
Tangu wakati huo, yamejengeka makundi ndani ya chama ambayo kwa kiasi
fulani yanamwona Nape na sekretarieti kama wafitini wanaojitwika jina
la mwenyekiti kuwashughulikia wengine.
Kwa hivyo, hata uamuzi wa Rais Kikwete kuwarejesha baadhi ya mawaziri
waliodaiwa na sekretarieti kuwa mizigo, unaelezwa kwamba huenda ukaibua
chuki kati ya mawaziri na Nape.
“Hivi hata ungekuwa wewe ni Nape, unapata wapi uhalali wa kuendelea
kuongoza watu ambao mwanzo uliwaona hawafai kiutendaji, lakini sasa
wamerejeshwa na mkuu wakof?
“Hawa kwa vyovyote watamjengea Nape na sekretarieti yake chuki. Vile
vile watamdharau kama kiongozi wao kwa sababu ni mara ya pili sasa
anasigana na mwenyekiti wake,” alisema mwenyekiti wa CCM wa mkoa ambaye
aliomba kuhifadhiwa jina.
Hatua ya Rais Kikwete kuwateua watuhumiwa haiishii ndani ya CCM pekee
bali hata baadhi ya wabunge walidai kushangazwa na uteuzi wa Mbunge wa
Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula
wakati bado anatuhumiwa kuomba rushwa.
Juni 13, 2011, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David
Kafulila, aliwataja wabunge wawili wa CCM bungeni akidai waliomba rushwa
katika halmashauri ambayo hakuitaja.
Akichangia mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Kafulila aliwataja
Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel akidai kwamba aliwakamata wakiomba
rushwa kwa viongozi wa halmashauri.
Hadi sasa tuhuma hizo zimekaliwa na ofisi ya spika, huku Kafulila
akisisitiza kuwa kile alichokisema ni ukweli mtupu na kwamba ushahidi
wake alishaukabidhi, lakini anashangazwa na ukimya uliopo.
Baada ya Kafulila kuibua tuhuma hizo, Badwel alikumbwa tena na kashfa
nyingine baada ya kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), akidaiwa kuomba rushwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Bagamoyo.
Hivi sasa mbunge huyo anaendelea na kesi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
0 comments:
Post a Comment