Kesi ya maafisa wa zamani wa
serikali ya Malawi wanaodaiwa kuhusika katika wizi wa mamilioni ya dola
kutoka kwa hazina ya serikali inatarajiwa kuanza Jumatano.
Sakata hiyo ilifichuliwa kufuatia jaribio la
mauaji dhidi ya mkurugenzi wa bajeti, Paul Mphwiyo - ambaye ameripotiwa
alikuwa tayari kufichua kashfa kubwa zaidi.
Hii
imetambuliwa kuwa kashfa kubwa zaidi kuwahi kutoke nchini Malawi.
Kashfa hiyo inayojulikana kama Cashgate imevuruga uhusiano mzuri ulioko
kati ya Malawi na wafadhili huku raia wakikasirishwa na wizi huo wa mali
ya umma.
Kashfa hiyo inaanzia katika eneo la kompiuta
ambapo habari za siri kuhusu uwekaji fedha zimehifadhiwa. Maafisa kadhaa
wa Serikali wamekuwa wakitumia udhaifu fulani katika mpango wa uhifadhi
wa kopmiuta hizo na kuiba mamilioni ya pesa kutoka hazina ya Serikali.
Inadaiwa kuwa huenda Dola Milioni 250 ziliporwa kwa kuwalipa
wafanyabiashara kimagendo kwa huduma ambazo hazikutolewa kwa Serikali.
Habari za uporaji huo wa mali ya umma
zilifichuka wakati Mkurugenzi wa Bajeti katika Wizara ya Fedha, Paul
Mphwiyo, alipopigwa risasi Septemba mwaka 2013. Tukio hilo lilitekelezwa
siku chache kabla ya mfanyakazi wa Cheo cha chini Serikalini
alipopatikana na pesa taslimu ya Dola 300,000 katika buti ya gari lake.
Pesa nyingi zaidi zilipatikana na kupokonywa wafanyakazi wa umma
manyumbani mwao katika buti za magari yao.
Wafadhili waku wa taifa hilo walikasirishwa
pakubwa. Wamesitisha utoaji wa Dola milioni 150 wakisubiri
kufanya
uamuzi baada ya uchunguzi katika kashfa hiyo kufanywa. Zaidi ya asilimia
40 ya bajeti yote ya Malawi hutegemea wafadhili. Hata hivyo kungali
kuna matumaini kwa Serikali ya Rais Banda kwa sababu Shirika la Fedha
Duniani (IMF) limeamua kutoa kwa Serikali jumla ya Dola Milioni 20,
ambazo lilikuwa limezuilia. Matokeo ya uchunguzi wa awali, uliofanywa
kuhusiana na kashfa hiyo, kwa ushirika wa wataalamu kutoka Uingereza,
umekamilika lakini matokeo yake hayajatangazwa.
Hadi kufikia sasa polisi wameshikilia magari,
nyumba na afisi za washukiwa wote wa kashfa hiyo ya Cashgate. Kesi ya
wawili kati ya watu 70 ambao wameshtakiwa kufikia sasa itakapoanza juma
hili, wengi wanatarajia kuwa ukweli zaidi utafichuka mahakamani.
0 comments:
Post a Comment