Mwanasheria
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na
Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratius Munishi, wamewataka makada wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, Edward Lowassa
na Andrew Chenge, kuacha kutumia kigezo cha udini kutaka kuungwa mkono
kwenye harakati zao za kukimbilia Ikulu.
Lissu na
Munishi walitoa kauli hizo wakati wakimnadi mgombea udiwani wa Kata ya
Sombetini, Ally Bananga, kwenye viwanja vya Ngusero.
Lissu
alisema kuwa baada ya makada wa CCM kuona hawana sifa za uongozi
kutokana na kuwa si waadilifu wala wasafi kulingana na tuhuma za ufisadi
zinazowaandama, wameamua kukimbilia makanisani, wakiwashawishi viongozi
wa dini wawaunge mkono kwa kigezo kuwa ni Wakristo wenzao.
“Kuna makada
wengine wa CCM nao wanazunguka huko misikitini wakisema hii ni zamu
yetu sisi Waislamu, hivyo anashawishi wamchague kwa kigezo cha Uislamu
tu. Hawa watu wanasahau dini si kigezo wala sifa ya uongozi,
tuwakataeni, sijui wanalipeleka wapi hili taifa, zaidi wanatutafutia
machafuko, hawatufai wote hawa,” alisema Lissu.
Akizungumzia
muswada wa mabadiliko ya Katiba, Lissu alisema kuwa katiba inasema kuwa
nchi ni moja lakini kwa sasa kuna Maamiri Jeshi wawili, ambao mmoja ni
Mwenyekiti wa CCM, Kikwete na mwingine ni Makamu wake, Dk. Ali Mohamed
Shein, jambo alilosema kuwa ni hatari sana hasa ikitokea wakitofautiana
na kupishana kauli ilhali wote wana majeshi.
Kwa upande
wake Katibu wa BAVICHA, Munishi, alisema kuwa dawa za kulevya zimeathiri
kwa kiasi kikubwa wananchi hivyo vita yake inapaswa kuwa ya dhahiri na
ya dhati ili kuepusha madhara zaidi, hasa kwa vijana ambao ndio
waathirika wakubwa.
“Asilimia 35
ya wananchi wa Tanzania ni vijana ambao wengi wao kwa sasa
wanaangamizwa na dawa za kulevya, lakini inasikitisha Rais wetu Kikwete
alitutangazia kuwa anayo majina ya wauza dawa lakini hayataji,
kayakumbatia tu Ikulu, kama huu si usanii ni nini? Sasa tunamtaka
atueleze hao wauza dawa za kulevya ni kina nani, tofauti na hapo naye ni
mshirika wao, ndiyo maana hawataji,” alisema Munishi.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alisema kuwa endapo serikali
haitafanyia maboresho daftari la kudumu la wapiga kura kabla zoezi la
kukusanya maoni ya katiba halijafanyika, watarusha helikopta 10 kila
kanda ya chama hicho itakuwa na yake ili kuhamasisha wananchi
wasijitokeze kutoa maoni.
Alisema kuwa
haiwezekani serikali kucheza na haki za wananchi wake kiasi hicho,
kwani mara ya mwisho daftari hilo kuboreshwa ni mwaka 2010, jambo
alilosema kuwa linawanyima haki Watanzania waliotimiza umri wa kupiga
kura kama Katiba ya nchi inavyotaka.
Pia
aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea aliyesimamishwa na CHADEMA,
Bananga, awe diwani wao ili washirikiane kupigania na kusimamia
maendeleo ya kata yao, ambayo imekaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuwa na
diwani.
“Kama
mnaridhika na umeme wa mgawo mchague mgombea wa CCM, kama mnaridhishwa
na elimu inayotolewa kwa watoto na wadogo zenu kwenye shule za serikali
chagueni mgombea wa CCM. Kama mnaridhishwa na mgawanyo wa rasilimali ya
utalii, madini na gesi mchagueni mgombea wa CCM, lakini kama mnataka
mchapa kazi, mpigania haki za wanyonge, mpinga ufisadi na rushwa,
mchagueni Bananga kwa maendeleo ya kata yenu,” alisema Heche huku
wananchi hao wakipaza sauti kuwa wanamtaka Bananga.
0 comments:
Post a Comment