Tabia ya kutumia vitu vyenye kemikali bila ya ushauri wa
kitaalamu imeendelea kujijenga miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa dawa
ya malaria aina ya Metakelfin inatumika kutengeneza kipodozi cha
kurembesha nywele.
Matumizi hayo hatari ya Metakelfin yamegundulika
huku kukiwa na taarifa za maji ya betri za magari, kutumika kama
malighafi ya kutengeneza mkorogo unaotumiwa na baadhi ya wanawake
kuchubua ngozi zao.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni na shirika lisilo
la kiserikali la Envirocare linalojihusisha na mpango wa kupunguza
madhara yatokanayo na bidhaa za vipodozi kwa binadamu na mazingira,
umebaini dawa ya malaria aina ya Metakelfin ni mojawapo ya kemikali
inayotumika kienyeji katika kutengeneza kipodozi cha kurembesha nywele.
Kwa mujibu wa mtafiti Issai Sen’genge, Metakelfin
ni miongoni mwa kemikali inayotumika kutengeneza mchanganyiko wa
kulainisha na kurefusha nywele.
Alisema idadi kubwa ya waliohojiwa, waliitaja dawa
hiyo ya malaria kuchanganywa ndani ya dawa nyingine za nywele ili
kupata mchanganyiko ambao husaidia kurembesha nywele.
“Swali lilikuwa kama kuna vitu vinavyotumika
katika kutengeneza mchanganyiko wa kupaka kwenye ngozi au nywele,
waliohojiwa walikiri kuchanganya, Metakelfin, Jik, maji ya betri na
kemikali nyingine,” anasema Seng’enge.
Kwa upande wake, Maria Kimiro ambaye ni mmiliki wa
saluni ya wanawake iliyopo Makongo jijini Dar es Salaam, alikiri
kusikia matumizi ya vidonge katika vipodozi lakini hana uhakika wa aina
ya dawa hizo.
“Nakumbuka kuna mtu nimeshawahi kumsikia
anazungumzia vidonge katika masuala ya vipodozi, lakini sina uhakika
kama ndiyo hiyo Metakelfin au vidonge vingine,”anasema Kimiro.
Asha Rashidi mkazi wa Tabata jijini Dar es salaam,
alikiri kuwa katika kutafuta urembo wanawake wanatumia vitu mbalimbali
hata vinavyohatarisha maisha ili mradi kutimiza azma yao.
Anasema kuwa hali hiyo mara kwa mara imekuwa
ikisababishwa na kuiga au kusikia kutoka kwa wengine bila kufikiria
madhara ya ambacho anatarajia kukifanya.
“Binafsi sijawahi kutumia hiyo Metakelfin kwa kuwa nafahamu ni dawa ya malaria lakini naamini kuna watu ambao wanaweza kuichakachua kwa namna wanavyoweza wakidhani kwamba inaweza kuwa na matokeo mazuri kwenye ngozi au nywele,” alisema.
Mtaalamu wa masuala ya Afya, Samwel Shita alisema mchanganyiko
huo wa dawa unaweza kuwa na madhara makubwa katika ngozi ya mtumiaji
kutokana na kemikali zinazotengenezwa.
Anafafanua kuwa Metakelfin imetengenezwa kwa ajili
ya matumizi ya ndani ya mwili na endapo itatumika nje ya mwili, ina
uwezekano mkubwa wa kusababisha ngozi kubabuka au ugonjwa wa saratani.
“Metakelfin ina sulphur na dawa za nywele pia zina
sulphur ndani yake, endapo mchanganyiko wake utawekwa kwenye ngozi
kuna hatari ya kubabuka au kusababisha saratani, hilo linatokana na
kemikali hizo kuwaua bakteria wanaolinda ngozi,”alisema Shita.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza alisema licha ya kutofahamu
kuhusiana na mchanganyiko huo lakini lazima utakuwa na madhara makubwa
kwa mtumiaji.
“Sijawahi kusikia kuhusu hiki kitu lakini naamini
huo mchanganyiko utakuwa na matokeo ambayo yanaweza kumdhuru mtumiaji,
hii ina maana unajitengenezea bomu likulipue mwenyewe,” alisema.
Kuhusiana na utengenezaji wa vipodozi kienyeji alisema kuwa udhibiti wake unatokana na utashi wa mtu binafsi.
“TFDA inasimamia na kudhibiti vipodozi vilivyopo
dukani hilo la watu kujichanganyia na dawa nyingine wakiwa majumbani
mwao linatuwia vigumu mno ingawa tunajitahidi kutoa elimu na kuelezea
madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na michanganyiko hiyo na
vipodozi kwa ujumla,” alisema.
Mara kwa mara TFDA imekuwa ikifanya jitihada za
kuviweka wazi vipodozi vyenye kemikali ambazo zina madhara kwenye mwili
wa binadamu.
Vipodozi hivyo ni vile vyenye sumu ambavyo ni
pamoja na Carolight, inayotajwa kuwa na sumu kali zaidi pamoja na vile
vyenye madini ya zebaki au mercury, ikiwamo sabuni ya Jaribu na Mekako.
Vingine ni vile vilivyochanganywa na viambata sumu
kama Clobetasol na Betamethasone ambapo inatajwa pia krimu ya Amira,
Betasolna Skin Success.
Matumizi yaliyokithiri ya vipodozi vyenye kemikali
kwa wanawake husababishia kundi hilo kuwa katika hatari kubwa zaidi ya
kupata maradhi ya saratani, figo, ini, fangasi, mzio na hata kuzaa
watoto wenye mtindio wa ubongo au kupoteza maisha.
Aidha, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 55 ya
Watanzania hawana uelewa kuhusiana na vipodozi vilivyokatazwa kutumika
kutokana na kuwa na madhara kwa mwili wa binadamu.
Utafiti huo unaonyesha kuwa licha ya jitihada kubwa ambazo
zimefanyika katika kuviweka wazi na kupiga marufuku ya vipodozi vyenye
kemikali idadi kubwa ya Watanzania hawana taarifa za kutosha kuhusiana
na vipodozi hivyo.
Kutokana na hali hiyo watu wengi wanajikuta
wakitumia vipodozi bila kufahamu kuwa vina kemikali ambazo zinaweza kuwa
na madhara makubwa katika miili yao.
Kaimu Mkemia Mkuu wa Serikali, Sabanitho Mtega
anakiri kuwa kuendelea kutumika kwa vipodozi vyenye kemikali
kunatokana na baadhi ya watumiaji kutoelewa lugha iliyotumika nje ya
makopo hayo na wengine kutoelewa ni kemikali gani zina madhara katika
mwili wa binadamu.
0 comments:
Post a Comment