MSAJILI
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amekemea vurugu zilizotokea
Januari 6 na 7 mwaka huu maeneo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
alizodai kufanywa na wafuasi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe
na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Jaji Mutungi alisema
vurugu hizo zilisababisha uvunjifu wa amani, hali iliyolilazimu Jeshi la
Polisi kuingilia kati.
Jaji Mutungi alisema ametumia fursa hiyo ikiwa ni moja ya majukumu ya
ofisi yake katika kusimamia utekelezaji wa sheria namba 5 ya vyama vya
siasa ya mwaka 1992 na kanuni za maadili ya vyama vya siasa za mwaka
2007.
“Sheria hii na kanuni zake hizi inakataza vyama vya siasa kuruhusu
wanachama au mashabiki wake kujihusisha na vitendo vya vurugu na
uvunjifu wa amani wa aina yoyote,” ilisema taarifa ya Jaji Mutungi.
Msajili huyo aliutaka uongozi wa CHADEMA na Zitto kuwazuia wafuasi
wao kufanya vurugu na kueleza kwamba mwanachama au shabiki wa chama cha
siasa aelewe kuwa atawajibika yeye binafsi kwa uvunjifu wowowte wa
sheria za nchi.
Aidha, Jaji Mtungu alitumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari
kujiepusha na ushabiki wa migogoro ya ndani ya vyama vya siasa, na
badala yake watafakari kwa undani athari za taarifa zao kwa jamii kabla
ya kutoa taarifa kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment