WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya pikipiki
waliyokuwa wamepanda kugongwa na basi la Kampuni ya Mtei Express katika
Kijiji cha Kisasida, nje kidogo ya Manispaa ya Singida.
Ajali hiyo ilihusisha pikipiki T 368 BXZ Skygo na basi T 742 ACU Scania lililokuwa linatoka Singida kwenda Arusha.
Waliokufa katika ajali hiyo ambao walikuwa wakienda shambani ni
Stamili Shaban na Kasim Shaban waliofariki dunia eneo la tukio na Hamza
Shaban akifia katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwendesha pikipiki, Shaban Bunku, aliyekuwa
amepakia abiria watatu, alilipita basi hilo kisha kukata kona, hali
iliyosababisha kugongwa kwa nyuma na basi hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, aliyefika eneo
la tukio, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema baada ya ajali
wananchi walilichoma moto basi hilo.
Hata hivyo alisema gari la zimamoto lilifika na kufanikiwa kulizima kabla ya kuteketea kabisa.
Kamanda Kamwela aliwaaasa wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi ajali zinapotokea, badala yake watii sheria.
Alisema dereva wa basi hilo, Dismas Ludovick, mkazi wa Singida alikimbia baada ya ajali hiyo.
0 comments:
Post a Comment