Sunday, 5 January 2014

ASKARI WAWILI MBALONI KWA TUHUMA ZA KUTEKA GARI

Filled under:

Askari wenye cheo cha sajini katika  Gereza la Ruanda na polisi mwenye cheo cha konstebo  katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya, wamekamatwa kwa tuhuma za kushirikiana na watu wengine watatu, kwa kuteka gari  na kupora  fedha na mali  katika eneo la Mlima wa Kawetere, Barabara ya Mbeya-Chunya, juzi jioni.
 
Inadaiwa kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa walipora Sh3.5 milioni  na mabegi yaliyokuwa na  vitu mbalimbali.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki katika kupora mali ya mfanyabiashara Sheedhar Paupeleti (38) baada ya kuteka gari alilokuwa akisafiria akiwa na watu wengine wawili.
Habari zilisema katika tukio hilo, dereva wa gari hilo Ezekiah Matatira, alifungwa pingu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema majambazi hayo yalikamatwa baada ya polisi kwenda katika  eneo la tukio, kutokana na taarifa zilizotolewa na wananchi kwa njia ya simu.
Kamanda  Msangi alisema tukio hilo lilitokea saa 11.30 jioni na kwamba majambazi hayo walikuwa yanatumia magari mawili. Alisema katika eneo hilo,  gari moja lilizuia njia  huku majambazi wakidai kuwa wamepata pancha na kwamba lilipofika gari la wafanyabiashara lilishindwa kupita  na hivyo kulazimika kusimama.
“Waliposimama, majambazi walimkamata dereva na kumfunga pingu wakidai wao ni polisi na walikuwa katika eneo hilo kuwasubiri watu hao ambao wanatafutwa’,’ alisema.
Alisema majambazi hao walimfungua pingu dereva na kuondoka na mfanyabiashara pamoja na funguo za gari lakini baadaye walimtupa chini mfanyabiashara huyo.
Kamanda huyo alisema polisi walipopata taarifa walikwenda katika eneo la tukio na kuweka kizuizi  kimoja na baadaye  kurudi Mbeya  na kwamba kikosi cha kwanza kilipishana na majambazi waliokuwa wakirejea Mbeya, lakini  kwa bahati nzuri  kikosi cha pili kilikuwa karibu na kizuizi ambapo majambazi walipofika walikamatwa na askari wa pande zote.

0 comments:

Post a Comment