Sunday, 5 January 2014

SITTA AIASA CCM,PENGO NAYE ASEMA YAKE

Filled under:



Wakati baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakipinga mapendekezo ya muundo wa serikali tatu kwenye rasimu ya pili ya mabadiliko ya katiba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, amekitaka chama hicho kisiwe kichwa ngumu kupinga muundo huo mpya wa serikali.
 
Akizungumza msimamo wa chama chake kupinga serikali tatu na kutaka muundo wa serikali mbili uendelee, Waziri Sitta alisema CCM inakosea kung’ang’ania serikali mbili wakati Katiba ya Zanzibar imevunja uhalali na uwepo wa serikali mbili.

Akitolea mfano, alisema Katiba ya Zanzibar inataka miswada yote inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano iridhiwe kwanza na Baraza la Wawakilishi, jambo ambalo alisema si sahihi.

Alisema Katiba ya Zanzibar imefanya mambo mengi kuihalalisha Zanzibar kuwa nchi kamili bila ridhaa ya Tanzania Bara.

Sitta alisema ili kubaki na serikali mbili, lazima Zanzibar ikubali kuifumua katiba yake inayotoa mamlaka kamili kwa rais wa visiwa hivyo, jambo ambalo alisema Wazanzibari hawawezi kulikubali.

“Mimi nilipomsikiliza Jaji Warioba safari hii, jinsi alivyojenga hoja ya serikali tatu, nimeona kuna hoja za msingi sana zipo, kwa sababu kuna mambo makubwa na ya msingi yameshafanyika. Huwezi kupitisha katiba inayosema miswada inayopitishwa bungeni isifanye kazi Zanzibar hadi Baraza la Wawakilishi likae na kuridhia, ukishafika hapo, basi serikali tatu haziepukiki,” alisisitiza  Sitta.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka CCM katika vikao vyake kukubaliana na muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Mbali na kuunga mkono muundo wa serikali tatu,  Sitta alipinga Tanzania kuongozwa na marais watatu.

Waziri huyo ambaye amepata kuwa Spika wa Bunge, alisema anakubaliana na mawazo ya Tume ya Warioba ya kuwa na serikali tatu, lakini hakubali Rais wa Zanzibar na Tanganyika nao waitwe marais kama yule wa Muungano.

Sitta alisema kuwa ili serikali tatu zifanye kazi kwa kuheshimiana, kuwekeana mipaka, rais wa Tanganyika na wa Zanzibar, wapewe  majina na hadhi nyingine ili Tanzania iwe na rais mmoja tu wa Muungano.

“Niliposikia maoni na ufafanuzi wa kina jinsi serikali tatu zitakavyokuwa, nimekubaliana na mawazo ya tume kwamba tuwe na serikali tatu. Lakini kwa maoni yangu tuwe na amiri jeshi mkuu mmoja tu ambaye ni rais wa Muungano, maana hatuwezi kuwa na marais watatu kwenye nchi moja,” alisisitiza.

Waziri huyo mwandamizi wa Serikali ya Rais Kikwete, alitolea mfano wa Shirikisho la Afrika Mashariki (EAC), kwamba rasimu yake imependekeza kuwa na rais mmoja tu na si marais sita wanaounda shirikisho hilo.

Pia alipendekeza jina la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania libadilishwe na badala yake iitwe Shirikisho la Nchi za Tanzania.

Alisema Tume ya Warioba imefanya kazi kubwa na nzuri kwani rasimu ya pili imekwenda mbali kuangalia vitu kama zawadi za viongozi, jambo ambalo zamani viongozi waliona ni haki yao kupata zawadi za aina hiyo bila kujali kwamba hiyo ni rushwa.

Kwa mujibu wa Sitta, kuna mambo ya msingi ya kuendelea kujadili nje na ndani ya CCM nayo ni namna ya kuiendesha Serikali ya Muungano kwani kwa maoni ya tume, serikali hiyo itakuwa ikichangiwa zaidi na Tanganyika, jambo ambalo linaweza kuibua manung’uniko ya upande mmoja wa Muungano.

Aliwataka wana CCM na wadau wengine kuifanyia kazi kauli ya Rais Kikwete aliyokaririwa akisema kuwa vyama visipojali masilahi ya taifa katika mchakato wa katiba, katiba mpya itakwama na Watanzania watalazimika kuendelea kutumia katiba ya sasa.

Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema haungi mkono mfumo wa serikali tatu uliopo katika rasimu ya pili ya katiba.

Akizungumza jana katika ibada ya shukrani ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata), Kardinali Pengo, alisema kuwa kuundwa kwa serikali tatu kutasababisha gharama kwa serikali, hasa kwa kuzingatia kuwa taifa hili ni masikini.

Kardinali Pengo alisema kuwa taifa halina fedha za kuweza kuhimili uwepo wa serikali tatu, na mfumo huo unaweza kuchangia kuvunjika kwa muungano.

“Kama serikali hizo zitafanikiwa, basi kuna uwezekano wa kuvunjika kwa muungano na Zanzibar kuweza kujitenga… Hivi sasa kuna mtazamo tofauti kuwa Bara wanaona kama Zanzibar inategemea michango kutoka huko, sasa kama kuna kuanza kwa mfumo huo ni wazi kuna uwezekano wa kujitenga,” alisema.

Mbali na hilo, askofu huyo aliwataka wale wanaoonyesha nia ya kuwataka kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kuacha kufanya hivyo kwa kuwa hatua hiyo inaweza kuchangia kuwepo kwa mpasuko katika vyama vyao.

Alisema kuwa ni vyema viongozi hao kuwa na subira ili wakati utakapofika kuweza kuteuliwa na vyama vyao.

“Viongozi wa vyama vya siasa wanaoonyesha nia ya kutaka uongozi ni vyema wakawa na subira maana suala hilo litachangia kuwepo kwa migogoro na hata kuchangia mpasuko katika vyama vyao,” alisema.

1 comments: