Wakati Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akitaka waziri
anayehusika na kusimamia Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC)
achukuliwe hatua kutokana na zabuni yenye harufu ya rushwa, imebainika
kuwa hukumu iliyotolewa na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA),
imesema kampuni iliyoshinda zabuni hiyo ilishiriki kuandaa nyaraka za
zabuni.
Hukumu hiyo, ni ile inayohusu kampuni ya zabuni za kuandaa vifaa vya uchaguzi vya kielektroniki, ambayo Nec iliipa kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution, tenda hiyo iliyokuwa na thamani ya Sh126 bilioni.
Hukumu hiyo ya PPAA imefikiwa baada ya kampuni za M/S Morpho na M/S IRIS Corporation Technology kukata rufaa kupinga uamuzi wa NEC.
Akizungumza bungeni jana, Zitto alisema kuwa kampuni iliyoshinda zabuni hiyo, gharama yake kwa kutoa huduma hiyo ilikuwa juu ilihali kuna kampuni nyingine zilizokuwa na bei ya chini pamoja na sifa za kufanya kazi hiyo.
Zitto alisema hayo wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliyowasilishwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gosbert Blandess.
Akijibu hoja za zabuni hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Uratibu na Bunge) William Lukuvi alisema kuwa, PPAA ilibaini kuwa mchakato wa utoaji wa tenda hiyo ulikuwa na upungufu mkubwa na ndiyo maana ilibatilisha tenda hiyo na kuamuru mchakato wa kumpata mzabuni urudiwe.
“Hivi vifaa siyo vya kupigia kura, ni vya uandikishaji, mchakato wa kumpata mzabuni ndiyo uliobainika kuwa na tatizo, tume ya uchaguzi itachunguza kujua chanzo cha tatizo na ikibidi ichukue hatua,” alisema Lukuvi.
Mapema akitoa maelezo yake, Zitto alisema kuwa “Serikali itoe taarifa ndani ya Bunge, nini kilichotokea na ni moja ya pendekezo ambalo ninataka kamati ichukue ili wafanyie azimio ili waziri anayehusika na uchaguzi aje alitolee ufafanuzi nini kimetokea na hatua gani zimechukuliwa,” alisema Zitto.
Alisema wanafahamu mfumo huo uliowahi kutumika katika nchi za Malawi, Kenya na Ghana, umeleta matatizo kwenye nchi hizo.
Alitaka waziri anayehusika kuwajibika kwa kuleta taarifa bungeni ili wabunge waijadili na kuona nini kilichotokea.
Alisema ni vizuri katika mchakato wa jambo kama hilo, wadau wote ambao ni pamoja na vyama vya siasa washirikishwe katika hatua ya tathmini ili kuweza kujenga kuaminiana na kuleta mfumo mzuri.
Katika hatua nyingine, Godbless Lema ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini, ametaka majina ya watu walioficha fedha nje yatajwe.
0 comments:
Post a Comment