Friday, 13 December 2013

PINDA ASEMA YUPO TAYARI KUACHIA NGAZI

Filled under:



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amevunja ukimya na kusema yuko tayari kuachia ngazi endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo, atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.

Pinda aliliambia Bunge mjini Dodoma jana kwamba endapo Rais hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977

Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.

Katika swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.

Mbunge huyo alisema, katika ziara hiyo, Kinana alifuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro.

“Walipokuwa Mbeya wakifuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kinana alisema kuna baadhi ya mawaziri ni mzigo, wewe kama kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali unachukuliaje kauli hii?” aliuliza.

Akijibu swali hilo, Pinda alisema hata yeye ameyasikia hayo kwenye vyombo vya habari na kusema, kiutu uzima hawezi kutoa maoni yake kwa kuzingatia yale yanayosemwa kwenye magazeti.

“Sisi tunangoja arudi (Kinana) tukae naye ili tujue alichokuwa anasema hasa ni nini na ninaamini alikuwa na baadhi ya wizara kichwani kwake,” alisema Pinda bungeni jana.

Katika swali lake la nyongeza, Rukia alisema wakati wanachangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo Mbunge wa CCM alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.

“Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?” aliuliza Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20 hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki.

0 comments:

Post a Comment