Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, amesema sheria mpya dhidi ya dawa za kulevya ambayo Serikali inatarajia kuifikisha bungeni mwakani, itahamasisha watumiaji/wafanyabiashara wadogo wa dawa za kulevya kuwataja wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.
Aidha alisema sheria hiyo inatarajiwa kuanzisha kitengo maalum cha mahakama ambacho kitakuwa na kazi ya kusikiliza kesi zinazohusu dawa za kulevya ili kuharakisha usikilizaji wake.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari bungeni juzi kuhusu taarifa aliyoiwasilisha bungeni ya hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2012.
“Wafanyabiashara hawa wakubwa wa dawa za kulevya ni lazima wafichuliwe, ni hatari lakini lazima wafichuliwe,” alisema na kuongeza, “tunategemea zaidi ushirikiano wa wananchi kufanikisha azma hiyo.
Akizungumzia taarifa hiyo, Lukuvi alisema tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwapo nchini ambako ukamataji wa kiasi kikubwa cha heroine kwa mkupuo umeendelea.
Alisema kwa Januari mwaka jana, mkoani Lindi walishuhudia kukamatwa kwa kilo 211 za heroine ambacho ni kiasi kikubwa kabisa cha dawa hiyo kuwahi kukamatwa hapa nchini kwa mkupuo.
Alisema tukio hilo pamoja na mengine yanaashiria kuwa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya huingizwa nchini kupitia vipenyo mbalimbali vikiwamo vilivyo kwenye ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,400.
0 comments:
Post a Comment