Maombi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ya kuomba kufutiwa shtaka la kukiuka uamuzi wa mahakama, yamebaki njiapanda baada ya Jamhuri kuyawekea pingamizi la kisheria, ikiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iyatupilie mbali.
Sheikh Ponda, kupitia kwa Wakili
wake Juma Nassoro, aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya marejeo, akiiomba
mahakama hiyo ifanye marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Maombi hayo yalitarajiwa kuanza
kusikilizwa jana lakini, Serikali iliwasilisha pingamizi hilo la awali na hivyo
mahakama hiyo ikalazimika kuanza kusikiliza pingamizi hilo kabla ya kuendelea
na maombi ya msingi. Pingamizi hili liliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu
(PSA), Bernard Kongola.
Wakili alidai kuwa hati ya kiapo
inayounga mkono maombi hayo ni batili kwa kuwa ina kasoro za kisheria.
Alibainisha kasoro hiyo kuwa ni
kutokuwa na tarehe ambayo kiapo hicho kilitolewa na kwamba hakuna mahali
panapoonyesha kuwa msimamizi wa kiapo alikuwa akimjua mla kiapo na wala kueleza
kuwa mla kiapo alitambulishwa kwake na nani.
Wakili Kongola alieleza kuwa hata
kwenye hati ya kiapo iliyoko katika jalada lililoko mahakamani inaonyesha kuwa
kuna kasoro hizo na kwamba walijiridhisha hivyo baaada ya kudurusu katika
jalada hilo la mahakamani.
Mheshimiwa Jaji, dosari hizi
haziwezi kurekebishika, kwa hiyo maombi yote ni batili,” alisema Wakili
Kongola.
Hata hivyo, Wakili wa Ponda, Nassoro
alisema kiapo hicho ni sahihi na kimetimiza matakwa ya kisheria kwa kuwa nakala
aliyonayo inaonyesha kiapo hicho kilitolewa na Oktoba 8, 2013 na kwamba,
msimamizi wa kiapo alikuwa akimfahamu mla kiapo, ambaye ni Ubaidi Hamidu.
Pia wakili Nassoro alisema Serikali
haijatoa ushahidi mahakamani kuonyesha kuwa kweli ililuhusu jalada la mahakama
na kubaini kuwa hati hiyo iliyoko mahakamani ina dosari hizo wala kueleza ni
lini alifanya hivyo hivyo.
Akijibu hoja hiyo Wakili Kongola
alisisitiza kuwa kiapo hicho ni batili kama walivyojiridhisha kwenye jalada la
mahakama, Novemba 21, 2013, na kwamba wanao ushahidi wa kutosha katika hilo.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Rose Teemba anayesikiliza maombi hayo
aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 11.
0 comments:
Post a Comment