Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha
zimenusurika kuteketea baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya
vyumba vyake jana alfajiri.
Wakati hayo yakitokea, msuguano ndani ya chama hicho umeendelea kushika kasi
baada ya jana, Mwenyekiti wake Mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu kujiuzulu
akipinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe.
Moto Arusha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kwamba
walipata taarifa za kuungua kwa ofisi hizo zilizopo eneo la Ngarenaro saa mbili
asubuhi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa alisema chumba cha kompyuta
ambacho kina kumbukumbu za wanachama wote Kanda ya Kaskazini kimeathirika.
“Hii ni hujuma dhidi ya Chadema; watu hawa walipanda juu ya ukuta na kuingia
ndani kupitia kwenye dari kisha kuchoma moto ofisi,” alisema Golugwa.
Alisema vyumba viwili ndivyo, vimeungua kabisa na kwa bahati nzuri moto
ulishindwa kusambaa na kuzimika baada ya umeme kuzimwa. Katibu wa Baraza la
Wanawake Chadema (Bawacha), Wilaya ya Arusha, Happiness Chale ambaye aliwahi
kushuhudia tukio hilo alisema, mhudumu wa ofisi hiyo, Jenipha Mwacha alibaini
moto huo baada ya kusambaa na kufika katika maliwato. Alisema kwa kawaida ofisi
hiyo inalindwa na walinzi wa Red Brigade.
Polisi walifika mapema eneo hilo na kuweka uzio ili kuzuia watu kuingia
katika ofisi hizo pamoja na kuanza uchunguzi wa tukio hilo.
Wakati polisi wakiwa katika ofisi hizo, viongozi wa Chadema Mkoa na Wilaya
ya Arusha walikuwa wakitoa maelezo polisi kuhusiana na tukio hilo.
Mwenyekiti Singida
Huko Singida, Kitundu amejiuzulu nafasi hiyo jana huku akieleza kuwa chama
hicho kinakiuka misingi ya demokrasia.
Uamuzi wa Kitundu umekuja siku nne tu, tangu Mwenyekiti wa Chadema mkoani
Lindi, Ally Chitanda naye kujiondoa katika nafasi hiyo akieleza kuchoshwa na
uamuzi wa kikanda na kikabila unaoendelea ndani ya chama hicho.
0 comments:
Post a Comment