Dk Kigwangalla alisema jana kwamba, hakuridhika na majibu ya kamati hiyo
kuhusu sababu za kuitupa hoja yake, kwani wakati akiitoa alieleza sababu za
kisheria na kanuni zilizokiukwa na Makinda, hivyo alitaka kuelezwa sababu siyo
kukataliwa pekee.
Katika ufafanuzi wake jana, Dk Kigwangalla alisema: “Kanuni ya Bunge ya 137
Ibara ya kwanza inaeleza utaratibu wa mtoa hoja kuiwasilisha kwa maandishi kwa
Katibu wa Bunge, nimeletewa barua kutoka ofisi ya Bunge ambayo haijaeleza
sababu za hoja yangu kukataliwa.”
“Nimeipata barua ya kamati hiyo. Katika hoja yangu nilichambua ukiukwaji
uliofanywa na Spika Makinda kwa kutumia kanuni na sheria zilizopo, nilitarajia
hoja ingeletwa bungeni lakini wameikataa.”
Dk Kigwangalla alisema hivi sasa anapitia sheria na kanuni za Bunge ili
kuona uamuzi atakaochukua baada ya hoja yake kukataliwa.
“Ngoja napitia kanuni na sheria za Bunge, nitajua cha kufanya kuhusu hili
katika vikao vinavyoanza kesho (leo),” alisema mbunge huyo.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema taarifa kuhusu kukataliwa kwa
hoja hiyo inaweza kutolewa rasmi iwapo kamati itaona umuhimu wa kufanya hivyo.
“Kama kamati ingeridhika kwamba kuna hoja muhimu, ingependekeza suala hilo
kupelekwa bungeni, lakini ilipofanya uchambuzi haikuona umuhimu huo, sisi
tulishamwarifu mhusika,” alisema Dk Kashililah.
Miongoni mwa madai ya Dk Kigwangalla katika hoja hiyo aliyotoa katika
mkutano wa Bunge uliopita, ni kwamba Spika amekuwa akikiuka kanuni za Bunge kwa
kuzuia mijadala ya dharura na kutokutoa nafasi kwa hoja za wabunge kama kanuni
zinavyoelekeza.
Madai mengine ni kuzuia kwa mabavu majedwali ya mabadiliko ya sheria kwenye
kamati ya bajeti, kuvunja masharti ya kanuni ya 48 inayotoa maelekezo ya namna
ya kuwasilisha na kujadili jambo la dharura na kutumia madaraka vibaya kwa
kuvunja masharti ya Sheria ya The National Assembly (Adminishation) Act
(Cap.115) ya mwaka 2008.
Suala jingine ni kumteua Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, tofauti na kanuni zinazotaja wenyeviti
kuchaguliwa na wajumbe wa kamati.
Pia, wanadaiwa kulipwa posho ya Sh430,000 wakati kamati nyingine wamekuwa
wakipewa Sh130,000.
0 comments:
Post a Comment