Sunday, 8 December 2013

POLISI MKOANI KIGOMA IMEMSHAURI DR SLAA KUSITISHA ZIARA ZAKE

Filled under:



Polisi mkoani Kigoma, imemshauri, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa kusitisha ziara zake mkoani Kigoma kwa sababu za kiusalama.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia Makunja alisema jana: “Ni ushauri tu tunatoa kwa Dk Slaa kwamba anaweza kuahirisha kutokana na hali ilivyo hapa.” Hata hivyo, Kamanda Makunja alisema pamoja na yote hayo bado Polisi mkoani, Kigoma imejipanga imara kukabiliana na vurugu zozote zinazoweza kutokea katika ziara hiyo.

Lakini Dk Slaa alipoulizwa kuhusu ushauri huo alisema hawezi kufuta ziara hiyo na kusema hahofii chochote. Alisema na alishafahamu siku nyingi kuwa hayo yanayotokea. Juzi, vijana mbalimbali waliandamana kwa pikipiki na wengine wakitembea kwa mguu huku wakiwa na mabango kupinga ziara ya Dk Slaa Kigoma. Anatarajiwa kuwasili Kigoma Kaskazini keshokutwa.

Hatua hiyo ya kupinga ziara hiyo, imetokana na Kamati Kuu ya Chadema kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Wakizungumza baada ya maandamano yao yaliyoanzia Kijiji cha Mwandiga kilichopo Kigoma Kaskazini hadi Uwanja wa Mwanga Center, Kigoma, vijana hao walisema kundi hilo halimuungi mkono Dk Slaa.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema katika Kijiji cha Mwandiga, Mtoro Mvunye alisema: “Tumetoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Issa Machibya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma (RPC) Fraser Kashai kusitisha ziara hiyo mara moja.”

Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo juzi, Mvunye alisema hawataki kumwona Dk Slaa akifika katika Kijiji cha Mwandiga, Ujiji na Mwanga.

“Kwanza nampongeza Mkuu wa Mkoa na RPC kwa kusimamia vizuri maendeleo ya Kigoma, lakini nataka niwaeleze kwamba endapo hawatachukua hatua ya kumzuia Dk Slaa kuja hapa Kigoma, hawa watu wanatudharau sana sisi wa Kaskazini,” alisema Mvunye.

Alitoa wito kwa wanachama wa Chadema kutowapigia kura kuwachagua viongozi wote wa mikoa na majimbo walioonyesha kutomuunga mkono Zitto katika sakata hilo ambalo limesababisha mgawanyiko kwa baadhi ya mikoa.

0 comments:

Post a Comment