Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amedaiwa kutoroka usiku
Makao Vatican ili apate fursa ya kwenda kutoa misaada kwa walemavu na watu
wasiojiweza.
Tetesi za Papa Francis kuwatembelea maskini hao usiku kwa kujificha zimekuja
baada ya mahojiano yaliyofanywa na Askofu Mkuu, Konrad Krajewski ambaye kazi
yake kubwa ni kukusanya fedha toka kwa wasamaria wema na kuwapelekea maskini.
Imeelezwa kuwa Askofu Krajewski amekuwa akiambatana na Papa Francis wakati
mwingine na kwenda kuwapa misaada maskini maeneo ya vijiji, mjini Vatican.
Askofu Krajewski alisema tangu zamani alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la
Buenos Aires, Papa Francis amekuwa akipenda kwenda mijini nyakati za usiku na
kuwatembelea wenye shida mbalimbali.
“Amekuwa akionyesha dalili ya kupenda kunisindikiza kwenda kuwapa misaada
maskini, pindi nikiondoka kwenda kufanya kazi hiyo,” alisema Padri Krajewski.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo Papa aliwahi kwenda naye nje ya mji kwa ajili
hiyo, Askofu Krajewski, alisita kujibu swali hilo.
Wakati huohuo, gazeti la Huffington Post limeripoti kuwa walinzi wa Uswisi,
wamethibitisha kuwa Papa amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali usiku akiwa
amevalia mavazi ya kawaida ya wachungaji na kuwapa misaada, wanaume na wanawake
wenye shida mbalimbali.
Tangu kuteuliwa kwake, papa Francis amevipamba vichwa vya habari duniani
baada ya kuonekana akijaribu kuvaa kofia za polisi wa zimamoto, kuwaruhusu
vijana wadogo wa kiume kuibusu miguu yake na kuwapigia simu waumini wake na
kuzungumza nao.
Hivi karibuni, aliripotiwa katika vyombo vya habari akiwabusu na kuwafariji
waumini walemavu katika Kanisa la Mtakatifu Peter, huku taarifa nyingine
zikionyesha kuwa ametuma fedha zake binafsi kwa wahamiaji na wanaohangaikia
mafao yao.
Alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Papa Francis alifahamika kwa
kutoroka usiku na kuwatafuta watu, kuzungumza nao na wakati mwingine
kuwanunulia chakula.
Mapapa wengine waliopita pia wametajwa kutoroka usiku, kwa mfano papa John
wa X111 alikuwa na tabia ya kutoroka usiku na kwenda mitaa ya Rome kufurahia
uzuri wa jiji hilo, wakati Papa Pius wa X11alivalia kama Mfaransa wakati wa
Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kwenda mipakani kuwasaidia Wayahudi wa Kirumi
kisha kuwaweka katika sehemu salama.
0 comments:
Post a Comment