Sunday, 15 December 2013

KAULI YA PINDA HAINA MASHIKO

Filled under:



Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamemkosoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kutamani kung’olewa kwenye nafasi, wakidai kuwa kauli yake inaonyesha jinsi alivyo mpole na dhaifu kiutendaji .

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ayezungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu alisema kuwa kauli ya Waziri Mkuu Pinda imeonyesha kwamba ana tatizo la kutokujiamini.

“Kazi za Waziri Mkuu zinajulikana wazi kwamba ni majukumu mazito ikiwemo kusimamia utendaji wa Serikali kwa kila wizara, hivyo kusema asihukumiwe kwa sababu ya wizara chache zisizofanya vizuri, inaonyesha ameshindwa majukumu yake. Alichotakiwa kufanya kwa wizara hizo ni kumshauri Rais awaondoe madarakani wasiowajibika,” alisema.

Alisisitiza: “ Hatutegemei kumwona Waziri Mkuu akiingia kufanya kazi kwenye kila wizara, isipokuwa anatakiwa kumshauri Rais ili mambo yaende sawa.”

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema kuwa amekuwa akifuatilia kauli za Waziri Mkuu Pinda hata anapokuwa kwenye ziara za kikazi, ambapo amekuwa akitoa kauli za kuwabembeleza watendaji, hata wanapoboronga.

“Waziri Pinda ni mpole, amepatikana kutokana na mfumo mbaya wa upatikanaji wa mawaziri uliopo nchini. Kwa wenzetu, waziri mkuu huchaguliwa mtu aliye jasiri, anayeweza kuongoza nchi kwa kusimamia shughuli mbalimbali Rais ananapokuwa nje ya nchi,”alisema na kuongeza:

“Waziri Mkuu akiwa dhaifu ni tatizo, hatujawahi kuwa na waziri mkuu mzuri tangu alipokufa Moringe Sokoine mwaka 1984, yeye alikuwa tofauti. Huu ni wakati mzuri wa kuweka hata kwenye marekebisho ya Katiba, kiwepo kipengele cha sifa za mawaziri, kwa sababu, wapo wengine unashangaa hata kigezo kilichotumika kumpa nafasi hiyo lakini ukifuatilia ni urafiki.”

Naye Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema anaona alichozungumza Waziri Mkuu Pinda ni sawa kwa kuwa angeweza kutangaza kujiuzulu, lakini ametoa nafasi kwamba kama Rais atamwondoa au wabunge watapiga kura ya kutokuwa na imani naye atashukuru.

Juzi, akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa yupo tayari kuachia ngazi endapo tu Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa na kama itatokea hivyo, atamshukuru Rais kwa kumwambia, ahsante.

Pinda aliliambia Bunge kwamba endapo Rais hatafanya hivyo, bado wabunge wanayo mamlaka ya kikatiba ya kumwondoa kwa njia ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF) katika utaratibu wa Bunge wa Waziri Mkuu kujibu maswali ya papo kwa hapo kutoka kwa wabunge.

Katika swali lake, Mbunge huyo alisema; Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa akiwa jijini Mbeya kuwa wapo mawaziri mzigo katika Baraza la Mawaziri.

Katika swali lake la nyongeza, Rukia alisema wakati wanachangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, yupo Mbunge wa CCM alisema kuwa Pinda ni mzigo namba moja.

“Kuna mbunge, tena wa CCM, alinukuu kauli ya Katibu Mkuu wa CCM na akasema kama ni mawaziri mzigo basi mzigo nambari moja ni wewe Waziri Mkuu, unawaambiaje Watanzania?” aliuliza Rukia.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema yeye anasimamia wizara 20, hivyo kama wapo watakaomhukumu kwa wizara moja ama mbili kwa kutofanya vizuri basi watu hao watakuwa hawamtendei haki

0 comments:

Post a Comment