Mbozi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi,
Dk Charles Mkambachepa juzi alionja joto la jiwe baada ya Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahaman Kinana kumtaka arudishe haraka Sh209 milioni za Saccos
ya Chama cha Walimu zilizochukuliwa na halmashauri hiyo katika mazingira ya
kutatanisha kuanzia Mei mwaka huu.
Hali hiyo ilijitokeza juzi jioni wakati Kinana alipozungumza na baadhi ya
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi hususan walimu.
Dk Mkambachepa alilazimika kutamka wazi kwamba atahakikisha anawalipa fedha
zote ifikapo mwishoni mwa Januari mwaka ujao na kwamba juzi hiyo aliwalipa
zaidi ya Sh32 milioni kupunguza deni hilo.
Awali Kinana alipokea taarifa ya malalamiko lukuki ya walimu yakiwamo ya
madai ya zaidi ya Sh1 bilioni na pia halmashauri kuchukua Sh209 milioni za
makato ya walimu kwa ajili ya kurudisha mikopo ya Saccos.
Walimu walidai halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi mstaafu Edson Chelewa
ilichukua fedha hizo ikidai zinatumika katika masuala ya kumpokea Rais Jakaya
Kikwete kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kitaifa mkoani Mbeya.
Kutokana na kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM alisema huo ni uzushi wa hali ya
juu na kuitaka halmashauri hiyo kuacha mara moja tabia ya kuwaonea walimu kwa
kusingizia viongozi mambo mabaya ya fitina.
“Kuanzia sasa CCM imeamua kuingia kati kufuatilia matatizo ya walimu
yakiwamo madai yao na kwa kweli itahakikisha yanalipwa” alisema.
Awali akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Baraza la Kata, Kinana
aliwasihi Watanzania kuendelea kuiamini Serikali ya CCM akisisitiza inalenga
kuwatetea wanyonge na kuboresha maisha.
0 comments:
Post a Comment