Ili kufanikisha mkakati wake, chama hicho kikuu cha upinzani nchini,
kimewaomba wabunge wa CCM kuwapa ushirikiano katika mkakati wake wa
kuwawajibisha mawaziri hao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika aliwataja mawaziri hao kuwa ni wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi,
Dk Shukuru Kawambwa, Kilimo, Chakula na Ushirika,
Christopher Chiza na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Mnyika alisema Chadema kimefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa mawaziri hao
wameshindwa kusimamia wizara zao kikamilifu.
Aidha, hatua hiyo imekuja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye kukaririwa akilalamikia utendaji mbovu wa baadhi ya mawaziri hao.
Nape alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akiwataja Chiza, Malima na
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa na alimsafisha Dk Kawambwa na kudai kuwa
hakupaswa kuhusishwa na utendaji mbovu wa Kampuni ya Progressive iliyokuwa
imepewa kazi ya kujenga Barabara ya Namtumbo-Tunduru.
Aliwashukia Chizza na Malima kwa kushindwa kufika mkoani Ruvuma kusikiliza
kero za wakulima ambao alisema wanakabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwamo ya
pembejeo.
Katika maelezo yake ya jana, Mnyika amemwongeza Profesa
Muhongo na kusema
Chadema kitawatumia mawaziri wake vivuli wa Wizara za Nishati, Kilimo na Elimu
kuwasilisha udhaifu wa kiutendaji wa mawaziri hao.
Mnyika alisema uamuzi huo umekuja baada ya chama hicho kuzindua rasimu ya
Sera ya Mabadiliko na Tabianchi ambayo inasisitiza kuwa mabadiliko hayo kwa
kiasi kikubwa yanachangiwa na Serikali kushindwa kusimamia vizuri sekta ya
nishati na madini, mifugo na kilimo.
“Inatakiwa suala la mabadiliko ya tabianchi liingizwe katika mfumo wa elimu
yetu ikiwa ni pamoja na wananchi kuelimishwa. Katika kilimo na mifugo kuna
tatizo kubwa kwani ardhi inatumika vibaya na kusababisha mabadiliko makubwa ya
tabianchi lakini mawaziri na Serikali yao wapo kimya,” alisema Mnyika na
kuongeza:
“Tunawaomba wabunge wa CCM watuunge mkono wakati Chadema tutakapoanza
kuwashughulikia mawaziri hawa. Wabunge hawa wanatakiwa kudhihirisha kuwa wana
uchungu na wasishindwe kama ambavyo wameshindwa kushughulikia ufisadi na rushwa
ndani ya chama chao.”
Mnyika alisema ni aibu kwa Kinana kuwataka mawaziri kuwajibishwa halafu
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akakaa kimya bila kuchukua hatua
yoyote... “Tunataka Rais Kikwete aseme chochote katika hili. Jambo la kuwang’oa
mawaziri hawa si la kuzungumzwa jukwaani, linatakiwa kuletwa bungeni kwa sababu
Bunge ndicho chombo kinachoweza kuibana vilivyo Serikali.”
0 comments:
Post a Comment