Polisi mkoani Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa
Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama wa
chama hicho ndio waliohusika.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amepinga kauli
hiyo na kulipa jeshi hilo siku nne kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa watano
baada ya kulipatia majina hayo akidai kuwa ndio wanaohusika na uchomaji moto
ofisi za chama hicho.
“Tumewapatia polisi majina... tunaamini walihusika moja kwa moja la sivyo,
chama kitatumia vijana wetu wa Red Brigade kuwakamata na kuwafikisha polisi,”
Lema aliwaambia waandishi wa habari jana.
Ofisi cha Chadema zilizoko katika eneo la Ngarenaro, zilinusurika kuteketea
kwa moto juzi baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya vyumba
vyake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi
mkoani Arusha, Japhet Lusinga alisema:
“Katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa hakuna mahali palipovunjwa kutoka nje
ya uzio na kuruhusu watu kuingia ndani... tumegundua kuna tundu dogo darini
eneo la kuelekea bafuni la upana wa futi moja na nusu kiasi haliwezi kuruhusu
mtu kupita.
“Tumejiridhisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupita hapo na ndani tulikuta
majivu na baadhi ya vitu vilivyoungua na vifaa vingine.”
Lema akiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro
alisema: “Tumebaini polisi wanataka kulifanya jambo hili kama la siasa ndiyo
sababu juzi badala ya kuanza kuchunguza waliohusika, waliwakamata Mtunza Ofisi
na mlinzi wetu na kuwalaza rumande hadi leo (jana) asubuhi kwa madai eti
wanawahoji.
“Hatukubaliani na taarifa yao, hii ni siasa. Kulitokea mauaji ya bomu,
wakasema Chadema wamejilipua, leo ofisi imechomwa wanasema Chadema wenyewe,
hili hatukubali, “ alisema.
Msajili alaani
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amelaani tukio la
kuchomwa moto ofisi hizo za Chadema na kusisitiza kuwa wananchi hususan
wanasiasa wasiwe wepesi kuingiza hisia kwenye makosa ya kijinai.
Alisema kuwa tukio hilo linapaswa kukemewa kwa hali yoyote ile kwa kuwa
linavuruga na kuhatarisha amani ya nchi.
0 comments:
Post a Comment