Mwisho wa mpaka wa ziwa nyasa
Malawi na Tanzania zimewasilisha ushahidi na majibu ya maswali kuhusu
umiliki wa maeneo kwenye Ziwa Nyasa, kwa jopo la wasuluhishi linaloongozwa na
Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano.
Wasuluhishi hao walizitaka Malawi na Tanzania kutoa majibu ya maswali manne
muhimu, wakati wakiwasilisha ushahidi wao kuhusu umiliki wa ziwa hilo wenye
mgogoro.
Mgogoro huo uliibuka baada ya Serikali ya Malawi bila kushauriana na
Tanzania kutoa leseni kwa kampuni mbili za kigeni, kutafuta mafuta katika eneo
la ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Malawi la Nyasa Times, msemaji wa
Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Malawi, Quent Kalichero
alithibitisha Jumatano wiki hii kwamba nchi hiyo imewasilisha majibu ya maswali
hayo na ushahidi uliohitajika.
“Waziri wetu amewasilisha taarifa maalumu ya maandishi kwa wasuluhishi na
kwa sasa yuko nchini Msumbiji, kwa ajili ya suala hilo,” alisema Kalichero
juzi.
Makabidhiano hayo yalifanyika mjini Maputo, Msumbiji ikiwa ni siku chache
baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mazungumzo na wasuluhishi, marais wa
zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano na wa Botswana, Festus Mogae jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza baada ya mkutano huo wa Jumatatu mjini Dar es Salaam, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe aliwaeleza
wanahabari kwamba mazungumzo baina ya Rais Kikwete na wasuluhishi hao yalihusu
zaidi ushahidi wa Tanzania katika suala la umiliki wa Ziwa Nyasa.
Pia alithibitisha kwamba Tanzania ilikuwa tayari kuwasilisha ushahidi
wake kwa sekretarieti ya ofisi ya waliokuwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika (SADC) inayoongozwa na Chissano, Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo wa Jumatatu, Membe alieleza kwamba nchi zote husika,
yaani Tanzania na Malawi zinatakiwa kuheshimu maagizo na kuwasilisha ushahidi
huo kwa wakati, na kuwaachia wasuluhishi kazi ya kupitia na kutekeleza wajibu
wao wakiwa wamepewa muda unaofikia mwaka mmoja kupata suluhu.
Wasuluhishi hao wa SADC, Chissano na Mogae waliwasili jijini Dar es Salaam
Jumapili iliyopita kwa ajili ya mazungumzo kuhusu mgogoro huo, kama
walivyofanya kwa Malawi Julai mwaka huu.
Julai mwaka huu, Rais Joyce Banda wa Malawi alinukuliwa akisema kuwa nchi
yake haina nia ya kulegeza kamba katika mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na
Tanzania.
Alitoa msimamo huo baada ya kukutana na Chissano wa Msumbiji na Thabo
Mbeki wa Afrika Kusini ambao ni wajumbe maalumu wa Jumuiya ya SADC katika
mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment